Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (Takukuru), wilayani Tunduru mkoani Ruvuma, vinawashikilia makarani na waandishi 11 wa vyama vya msingi kwa tuhuma za kununua korosho za wakulima kwa fedha taslimu katika vituo vya kukusanyia korosho.
Hatua hiyo imekuja baada ya Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro kuendesha oparesheni maalumu ya kupambana na biashara haramu ya korosho maarufu jina la kangomba.
Makarani na waandishi hao wanatuhumiwa kujihusisha na ununuzi wa korosho kwa fedha taslimu katika vituo vya kukusanyia korosho na kisha kuziingiza kwenye mfumo rasmi wa stakabadhi ghalani.
“Mmekuwa mkiwashinikiza wakulima wawaaachie korosho zao kisha mnawalipa fedha tasilimu shilingi 1,500 kwa kilo moja, na kisha korosho hizo mmekuwa mkiziingiza kwenye mfumo rasmi kwa kutumia majina ya matajiri waliowakabidhi fedha ili kufanya uhuni huo,” alisema DC Mtatiro katika kikao na viongozi na waandishi na makarani wa vyama vya msingi.
“Siyo tu kwamba mmeripotiwa na wakulima, bali hata korosho za mtego za DC zilipowafikia mlizinunua na ndipo tukabaini kuwa nyinyi ni vinara wa kuvunja viapo vyenu vya kazi kwenye vyama vya msingi,” alisema
Pamoja na kukamatwa kwa watumishi hao 11 wa vyama vya Msingi wilayani Tunduru, Mtatiro amewasimamisha majukumu hayo na kuwapiga marufuku kukihusisha na masuala ya korosho kwenye vyama vya msingi katika msimu huu.
Hata hivyo amewataka viongozi wa vyama vya msingi ambavyo watuhumiwa hao wanafanya kazi, viwaondoe kazini mara moja ifikapo leo
DC Mtatiro amechukua hatua hiyo alipokuwa akizungumza na viongozi, waandishi na makarani wa vyama vya msingi wapatao 500 katika ukumbi wa Cluster wilayani Tunduru na kusisitiza kuwa oparesheni kangomba ni endelevu.
Social Plugin