Polisi wilayani Hai wamemkamata mwenyekiti wa Halmashauri ya Hai (Chadema), Helga Mchomvu kwa amri ya mkuu wa Wilaya hiyo, Lengai Ole Sabaya.
Sabaya amethibitisha kukamatwa kwa Mchomvu leo Alhamisi Novemba 14,2019 na kumtaka mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kujisalimisha akidai alifanikiwa kutoroka.
"Ndio tumemkamata mwenyekiti na watu wengine wawili lakini Lema nimeambiwa alifanikiwa kutoroka kupitia mlango wa nyuma na kutelekeza gari lake aina ya Toyota Landcruicer," alisema Sabaya.
Sabaya amedai kiini cha kuagiza viongozi hao wakamatwe ni kutokana na kile alichokiita kuendeleza njama zao za kuvuruga amani katika wilaya hiyo na kusababisha taharuki kwa wananchi kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
"Kitendo cha mbunge Lema kutoka Arusha na kuja hapa Hai na kufanya vikao vya siri ni sawa na kuvuka mstari mwekundu na hili sisi kama Serikali hatuwezi kulivumilia. Namtaka Lema ajisalimishe mwenyewe polisi," amesisitiza Sabaya.
Social Plugin