Msanii wa vichekesho, Idris Sultan amemuomba radhi Rais Dk. John Magufuli kwa kitendo cha kufanyia ‘photoshop’picha yake akidai alifanya vile kwa dhumuni la kumtakia kheri ya siku ya kuzaliwa kwa kutumia sanaa ya uchekeshaji ambayo ndiyo anayoitumia kufanya kazi zake.
Idris ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Novemba 14, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ambapo amesema kuwa amepitia mafunzo ya jeshi na kwamba anauelewa uongozi mzima hivyo hawezi akawa mmoja kati ya watu wanaotaka kumkebehi rais.
“Katika hali ya ubinadamu tukiachana na sheria kama picha ile ilimkera na hajapenda kwa namna nilivyomtakia kheri katika hali ile sina budi kumuomba radhi kama babaangu na kiongozi wangu kwani sikuwa na nia mbaya bali ilikuwa kufurahisha watu lakini bahati mbaya safari hii imechukuliwa katika hali ya tofauti na watu wengi sana tumeshtushwa na tunaiacha sheria ichukue mkondo wake.
“Hiki kitu kimeathiri sana kazi yangu kwasababu sina simu yangu wala kompyuta yangu na hivyo ndio vitendea kazi vyangu vikubwa, watu wengi waliokuwa wakinitafuta kwa ajili ya kufaya kazi imebidi zipelekwe mbele na hii imetokana na kutoeleweka nia yangu ni nini,” amesema Idris.
Ameongeza kuwa askari wamemuonesha ushirikiano wa kutosha kwenye jambo hilo ikilinganishwa na namna alivyotarajia akitolea mfano mitazamo tofauti ya watu wanaosema kuwa unapoenda kituo cha polisi kabla haujaanza kuzungumza ni lazima upigwe vibao kwanza lakini kwa upande wake haikuwa hivyo.
Social Plugin