Kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS limemtangaza kiongozi wake mpya baada ya kuthibitisha kifo cha kiongozi wake Abu Bakr al-Baghdadi katika shambulizi lililofanywa na Marekani nchini Syria.
Taarifa iliyotolewa kwenye chombo cha habari cha IS, al-Furqan imeeleza kuwa nafasi ya al-Baghdadi itazibwa na Abu Ibrahim al-Hashimi al-Qurayshi.
Kundi la IS halikutoa taarifa zaidi kuhusu al-Qurayshi. Kiongozi huyo mpya anatambuliwa kama msomi, shujaa mashuhuri na kiongozi wa kivita ambaye amepambana na majeshi ya Marekani na ana ufahamu kuhusu vita hivyo.
Taarifa hiyo pia imethibitisha kifo cha Abu Hassan al-Muhajir, msaidizi wa karibu wa al-Baghdadi ambaye alikuwa pia msemaji wa IS tangu mwaka 2016.
Vifo hivyo ni pigo kubwa kwa kundi la Dola la Kiislamu karibu miezi saba tangu lilipofurumushwa kutoka kwenye ngome yake ya mwisho nchini Syria.
Social Plugin