Kamanda wa Polisi Tarime/Rorya Henry Mwaibambe akionyesha silaha iliyokamatwa na Polisi wakati wakikabiliana na watuhumiwa wa ujambazi
Na Dinna Maningo - Malunde 1 blog Tarime.
Watu watatu wanaotuhumiwa kwa ujambazi wameuawa wakati wakijaribu kuwashambulia askari polisi kwa risasi katika kijiji cha Obwere -Shirati wilayani Rorya mkoani Mara.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Polisi Tarime /Rorya Henry Mwaibambe amesema tukio hilo limetokea Novemba 7 ,2019 majira ya saa nne usiku baada ya watuhumiwa hao walipovamia nyumbani kwa David Ogutu maarufu (Baba Ouma)kwa lengo la kutaka kuiba mali.
Alisema k katika mashambulizi hayo polisi walifanikiwa kuwanyang'anya silaha mbili aina ya AK 47 ikiwa na risasi tano na nyingine ya Kienyeji ambayo maganda yake hayajapatikana.
"Walivamia majambazi watano ila kwa bahati nzuri Ogutu alipiga simu Polisi na polisi waliwahi eneo la tukio na ndipo majambazi wakaanza kuwarushia polisi risasi, Polisi nao wakajihami na hivyo kufanikiwa kuwajeruhi watatu ambao walipoteza maisha na wawili wakakimbia,tunawatafuta",alisema.
"Mmoja aitwae Kisante Chacha (19)yeye alikimbia akiwa amejeruhiwa na kutoka damu tulimkamata akiwa kapanda gari zinazokwenda Sirari maana tulikuwa tulishawajulisha wananchi popote watakapoona mtu ana majeraha ya damu watoe taarifa na wakatupa ushirikiano,nguo zilikuwa na damu kutokana na majeraha ya risasi",alisema Mwaibambe.
Kamanda huyo alieleza kuwa mtuhumiwa huyo alifariki kutokana na kuvuja damu nyingi huku John Marwa ambaye nae alikuwa amejeruhiwa kwa risasi alikutwa kwenye nyumba ambayo haijaisha akiwa amekufa.
"Mwaka juzi kama tulivyosikia kwenye vyombo vya habari kuwa Mwanamke kapambana na Jambazi alikuwa ni huyu Kisante, tulimkamata akafikishwa mahakamani kwa kuwa umri wake ulikuwa chini ya miaka 18 alifungwa kifungo cha nje na baadae akaendelea na vitendo vyake viovu.
Mwaibambe amewashukuru wananchi wa Rorya na Tarime kwa ushirikiano wao ambao ulifanikisha kuwakamata baadhi ya waharifu huku akiwataka vijana kutafuta mali kwa njia halali.
Social Plugin