Mhadhiri wa Chuo Cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Samson Mahimbo (69), amehukumiwa kulipa faini ya TSh. Milioni tano au kwenda jela miaka mitatu baada ya kukiri mashtaka yaliyokuwa yakimkabili ikiwemo kuomba rushwa ya ngono kutoka kwa Mwanafunzi wake Victoria Faustine.
Hukumu hiyo imesomwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya mshtakiwa kuingia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) ikiwamo kuomba msamaha na kukiri makosa yake.
Hakimu Shaidi amesema tabia ya rushwa ya ngono inaongezeka na ni gumzo katika vyuo hapa Nchini na kwamba inapaswa kukemewa na kusema kitendo alichofanya mshtakiwa huyo ni cha aibu kwa umri wake kwani mtu wa Taaluma yake alipaswa kuwa mfano wa kuigwa lakini akaamua kujiingiza katika mapenzi na Watoto wadogo ambao si hadhi yake.
Akitoa utetezi wake, kabla ya kusomwa kwa hukumu hiyo, Wakili wa utetezi, Claudia Msando amedai mshtakiwa ana umri mkubwa na kwamba ameshaanza kupata maradhi yaa uzee ikiwamo kutokusikia na kuona vizuri na pia ni Mstaafu na ana familia inayomtegemea.
Hata hivyo, Mhadhiri huyo bado hajalipa faini hiyo yote bali amelipa Tsh.Milioni mbili baada ya makubaliano hayo na yuko nje akitakiwa kuhakikisha anamaliza kulipa.
Social Plugin