Vyombo vya habari vya Urusi vimeripoti kuwa mwanaume mmoja mjini Moscow anakabiliwa na kifungo cha miaka mitano kwa kosa la kumtumia paka 'nyau' kama silaha yake.
Mtuhumiwa huyo Gennady Shcherbakov anatuhumiwa kwa kumrushia polisi paka wakati ambapo polisi alikuwa ameenda kuthibiti kelele ambazo zilikuwa katika makazi ya watu.
Bwana Shcherbakov, 59, anakabiliwa na kosa la jinai la unyanyasaji dhidi ya polisi.
Kesi hiyo ilifunguliwa siku ya jumatano, ambapo ilikuwa ni kipindi cha zaidi ya mwaka tangu tukio hilo litokee , imeripotiwa na chaneli ya Telegram Baza
Tuhuma hizo zilikuwaje?
Kwa mujibu wa televisheni ya taifa ya Urusi, tarehe 4 oktoba 2018, bwana Shcherbakov alikuwa amekuwa anapiga kelele katika makazi ya watu huko Moscow.
Anadaiwa kuwa alikuwa amelewa sana.
Wakazi wa eneo hilo waliripoti kuhusu usumbufu aliokuwa anasababisha.
Mara baada ya polisi kufika katika eneo hilo kumzuia asiendelee kufanya fujo , bwana Shcherbakov aligoma kutoa ushirikiano kwa polisi na hata kujibu maswali aliyokuwa akiulizwa.
Badala yake bwana Shcherbakov anadaiwa kuwa alimnyanyua paka ambaye alikuwa karibu yake na kumrushia polisi.
Mnyama huyo anaripotiwa kuwa alimjeruhi polisi.
Bwana Shcherbakov, ambaye hakuwa mkazi wa eneo hilo, anakanusha kuhusika na tukio hilo na hata kutumia paka kama silaha.
Yeye anadai kuwa paka huyo alimrukia polisi mwenyewe bila kurushwa au kusukumwa na mtu yeyote.
Kesi hiyo imewekwa kwenye kifungu cha 318 , kwa kosa la uhalifu wa jinai wa kutumia vurugu dhidi ya asifa wa umma.
Haijafahamika kwa nini kesi hiyo imechukua muda mrefu kufunguliwa kama kosa la jinai na hata hawajaeleza nini kitamkuta paka aliyehusika
Chanzo - BBC