Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza Wizara ya Fedha na Mipango kutoa shilingi Bilioni 40 kwa ajili ya kumalizia madeni yote ya wakulima wa korosho yaliyobaki baada ya Serikali kununua korosho za wakulima katika msimu wa mwaka 2018/19.
Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo Ikulu Jijini DSM alipokutana na viongozi wa Wizara, Mikoa, Wilaya na Taasisi za Serikali ambazo zinahusika katika uzalishaji na mauzo ya zao la Korosho.
Mkutano huo umehudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Majaliwa.
Pamoja na kuagiza Wizara ya Fedha na Mipango itoe fedha hizo kesho tarehe 02 Novemba, 2019 Rais Magufuli amewaagiza viongozi wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha fedha hizo zinawafikia wakulima na sio vinginevyo, na pia kuhakikisha wanalipwa wakulima wanaostahili kupata malipo hayo.
Rais Magufuli ameelezea kutoridhishwa kwake na utendaji kazi wa Wizara ya Kilimo na viongozi wa Mikoa na Wilaya ambao katika maeneo yao kumetokea wizi mkubwa wa fedha za wakulima kupitia vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) hali iliyosababisha wakulima wengi kuishi maisha duni.
Rais Magufuli amesema amesikitishwa kuona viongozi wa Wizara, Mikoa na Wilaya hawajachukua hatua madhubuti dhidi ya watu wanaowaibia wakulima mpaka alipoamua kumtuma Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Brig. Jenerali John Mbungo ambaye kwa muda mfupi amebaini kuwepo wizi wa shilingi Bilioni 1.23 na tayari amefanikisha kurejeshwa kwa shilingi Bilioni 375 katika Mkoa wa Lindi pekee.
Amewataka viongozi wa Wizara ya Kilimo, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kubadilika na kuhakikisha haki za wakulima zinalindwa ipasavyo kwa kurejesha fedha zilizoibwa na kuzuia mianya yote ya wizi.
“Nataka mfanye kazi, hakuna mtu wa kuwanyanyasa, nendeni mkashughulikie kero za wakulima, mna vyombo vya ulinzi na usalama nendeni mkavisimamie, kinyume na hapo nitakuona hutoshi kwenye nafasi hiyo” Rais Magufuli.