Rais wa Tanzania, John Magufuli amemwagiza Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma (DED), Godwin Kunambi kuanza kuwalipa wananchi fidia zao Desemba Mosi, 2019 ili kupisha ujenzi wa Makao Makuu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Rais Magufuli ameyasema hayo leo Jumatatu Novemba 25, 2019 jijini Dodoma wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa makao makuu ya JWTZ yatakayojengwa katika eneo la Kikombo jijini humo ikiwa ni mwendelezo wa serikali kuhamia Dodoma.
Amemtaka Mkurugenzi wa Jiji kubeba jukumu la kuwalipa wananchi 1500 wanaoondolewa kwenye eneo hilo jumla ya Sh3.399 bilioni kwa sababu jiji hilo litanufaika kwa JWTZ kuhamia Dodoma na wananchi hao pia ni wakazi wa Dodoma.
Aidha amewataka wananchi wanaostahili kulipwa fidia kuacha kuwasikiliza matapeli wanaowadanganya kuwa ndio wenyeviti wanaosimamia mafao yao na badala yake wahakikishe wanaenda kuchukua fedha zao ifikapo Desemba Mosi mwaka huu kwani mtetezi wao ni serikali na sio mtu mwingine yeyote.
“Kwasababu jiji la Dododoma liko pale kwa kujibu wa sheria na ninafurahi kwamba Mkurugenzi ambaye ni kijana amekuwa akiongoza kwenye makusanyo katika jiji hili ninatoa maelekezo leo kwa Mkurugenzi wa jiji achukue bilioni 3.399 kuanzia Desemba Mosi mwaka huu aanze kuwalipa fidia wananchi wa hapa bila kuwapunja.
“Ninatoa wito kwa wananchi wanaopaswa kulipwa fidia msianze kubadilisha hizo fidia maana ninafahamu kuna matapeli ambao wanapita kwenye maeneo yenu wakijiita kuwa ndio wenyeviti wa kutete fidia embu achaneni nao maana mtetezi ni serikali wala wasije wakawadanganya kwani wa kufanya hivyo mnajichelewesha.
Ameongeza kuwa kwa wale watakaojichelewesha kuchukua fidia hiyo ninajua wanajeshi wakishaingia rasmi katika eneo hilo itabidi waende kuwaomba wao mwenyewe.