Rais Magufuli amesema kuwa askari polisi wanaoishi kwenye nyumba za jeshi nchini kuanzia sasa hawatatozwa tena kodi ya nyumba na hivyo amewataka kukaa kwa usalama na kwamba serikali italibeba deni hilo akidai walikosea kusaini mkataba uliowataka askari hao kulipa kodi.
Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Novemba 25, alipokuwa akizungumza kabla ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa Makao makuu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
“Kwa mkataba ambao tulisaini sisi wenyewe ni kwamba nyumba za wanajeshi zikijengwa watakaokuwa wanakaa huko watakatwa lakini ukweli ni kwamba hauwezi ukawachukua askari wanaokaa kwenye nyumba ambazo ni kama mahanga halafu uanze kumtoza fedha, ninafahamu deni hilo ni kubwa lakini ninawahakikishia kuwa katika nyumba zote zilizojengwa nchi nzima ambao mkataba wake ulisema wanaokaa mule wakatwe hakuna kukatwa askari yeyote hilo deni litabebwa na serikali.
“Kabla sijaja hapa nimeshamwelekeza Waziri wa Fedha na Katibu Mkuu na ninafikiri kesho au keshokutwa wataanza kulilipia hilo deni ambalo limeiva na wataanza kulipa zaidi ya Dola za Marekani milioni 25 kwani deni lenyewe ni kubwa zaidi ya Sh trilioni moja lakini siwezi nikawaweka maaskari wangu kwenye utumwa wa nyumba za kulala.
“Badala ya kulala ukaota mabomu na namna ya kupiga risasi unaanza kuota jinsi ya kulipa deni la nyumba kwa wakati wangu hilo hapana, ni kweli mkataba ulikosewa lakini siwezi nikakubali makosa ya namna hiyo yakaanza kufanyika katika kipindi changu kwahiyo maaskari mnapoingia kwenye nyumba zenu kama una mke wako lala salama,” amesema Rais Magufuli.