Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI KUMEGA EKARI 3000 KUTOKA KWENYE SHAMBA LA KARAMAGI KILOSA

Na Farida Saidy- Morogoro.
Serikali ya awamu ya tano kupitia Wizara ya Ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi imeagiza mmiliki wa shamba la Farm Africa maarufu kama shamba la Karamagi lililopo katika Halmashauri ya Wilaya Kilosa Mkoani Morogoro kutoa ekari 3000 kutoka kwenye shamba hilo ili zimilikishwe kwa wananchi wenye uhitaji wa ardhi kwa shughuli za kiuchumi.


Agizo hilo la Serikali limetolewa Novemba 8 mwaka huu na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi alipotembelea shamba hilo lenye ukubwa wa ekari elfu 13 ambapo hakuridhishwa na kasi ya uendelezaji wa eneo hilo tangu Mmiliki wa shamba hilo alipomilikishwa.

“Kwa taarifa zilizopo bwana Karamagi alimilikishwa shamba hili tangu mwaka 2012, hivyo alipaswa kila mwaka kuliendeleza shamba lake japo kwa kiwango cha moja ya nane (1/8), hii ina maana hadi kufikia mwaka huu ambapo umiliki wake umetimiza miaka minane alipaswa kukamilisha uendelezaji wa eneo hili” alisema Waziri Lukuvi,

“Kutokana na hali hii nikuagize Mkuu wa Wilaya umfikishie taarifa bwana Karamagi kwamba mimi kama Waziri wa Ardhi namuagiza atoe ekari 3000 kutoka kwenye shamba hili ili zimilikishwe kwa wananchi ili waziendeleze kwa shughuli za kilimo”, alisisitiza Waziri Lukuvi.

Sambamba na agizo hilo, Waziri Lukuvi alibainisha kuwa 2012, ni ekari 2000 pekee ndizo zilizoendelezwa kwa kupanda mazao kati ya ekari 13,000 za licha ya kipindi cha miaka minane kupita tangu mmiliki huyo alipopata uhalali wa eneo hilo mnamo mwaka shamba hilo wakati alitakiwa awe ameendeleza shamba lote kwa kipindi hicho.

Awali, kabla ya kutoa uamuzi wa kumega sehemu ya shamba hilo ekari 3000, Mhe. Lukuvi alisikiliza kero za wananchi wanaoishi jirani na shamba hilo ambao wengi walimuomba kuwasaidia kupata maeneo kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kilimo wakitaja shamba hilo kuwa ni sababu kubwa ya kuwakosesha maeneo ya kulima
Akiongea na viongozi wa Wilaya ya Kilosa katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo, Mhe.Lukuvi alibainisha kwamba Serikali tayari imejiridhisha kuwepo uhalali wa kufutwa mashamba 48 yaliyopo katika Halmashauri hiyo ambayo hayajaendelezwa ili yagawiwe kwa wananchi wa Wilaya hiyo kwa ajili ya kuyaendeleza.

Aidha, amewataka viongozi wa Halmshauri hiyo kufuatilia mashamba mengine 24 ambayo yameonekana kutoendelezwa ili waandike ilani kwa ajili ya kuomba kufutwa na kugawiwa wananchi wenye uhitaji.

Katika hatua nyingine Waziri Lukuvi amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi kuhakikisha suala la udalali na ukodishaji wa ardhi unaofanywa na baadhi ya viongozi wa Wilaya hiyo na kuwakosesha wananchi maeneo ya kilimo unakoma mara moja kwani suala hilo linapelekea kuibuka kwa migogoro ya ardhi Wilayani humo.

Sambamba na hayo Waziri Lukuvi amewaagiza wataalamu wa ardhi kuepuka kubadilisha hati za umiliki wa ardhi kwa wananchi watakaogawiwa maeneo yanayotokana na mashamba yaliyofutwa huku akiwataka wananchi kutouza maeneo watakayopewa kwani hiyo ni huruma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli.
Akiendelea kutoa maagizo mbalimbali, Waziri Lukuvi amewataka wafugaji wote waliomilikishwa ardhi kihalali Wilayani Kilosa kuweka uzio katika maeneo yao ili kuzuia mifugo isitoke katika maeneo yao na kuingia katika maeneo ya wakulima ili kuepuka migogoro ya Mara kwa mara.

Amesema wakati umefika sasa kwa wafugaji kuacha ufugaji wa kizamani badala yake watumie maeneo hayo kufuga mifugo yao kisasa ndani ya eneo lenye uzio ili mifugo yao iwe na tija zaidi kwao ukilinganisha na ilivyo sasa.
Waziri Lukuvi yupo Mkoani Morogoro kwa ziara ya kikazi ya siku mbili ikiwa na lengo la kupata maoni na mapendekezo juu ya kazi ya awali iliyofanywa na tume ya uhakiki wa mashamba yasiyoendelezwa huku akishangazwa na upendeleo ulioonyeshwa katika kuyabakiza mashamba 24 ambayo yameonekana bado hayajaendelezwa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com