Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb)
Na. Peter Haule, WFM, Dodoma
Serikali imefanikiwa kuwarejeshea wafanyabiashara na wawekezaji Kodi ya Ongezeko la Thamani-VAT baada ya uhakiki wa madai yao kwa lengo la kuimarisha kipato cha mtu mmoja mmoja na uwekezaji nchini.
Hayo yamesemwa bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti maalum, Mhe. Khadija Nassir Ali, aliyetaka kujua namna Serikali ilivyojipanga kurejesha Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa wawekezaji ili kuimarisha uwekezaji.
Dkt. Kijaji alisema kuwa, Serikali imelipa zaidi ya asilimia 90 ya VAT kwa watu waliokuwa wakidai Serikali baada ya kufanyika kwa uhakiki wa madai hayo, uhakiki unaendelea kwa asilimia kumi iliyobaki ili kujiridhisha kabla ya kufanya malipo.
“Tulikua na changamoto kubwa ya udanganyifu kwenye eneo la urejeshwaji wa Kodi ya Ongezeko la Thamani, hivyo Serikali ilianza mkakati wa kujiridhisha na kila muamala unaoletwa ili kuweza kuirejesha kwa wazalishaji, wanunuzi pamoja na viwanda vilivyopo nchini”, alieleza Dkt. Kijaji.
Aidha, akijibu swali la Msingi la Mbunge wa Busega, Mhe. Dkt. Raphael Chegeni, aliyetaka kujua maana ya dhana ya ukuaji wa uchumi kwa kuoanisha na Maisha ya wananchi, Dkt. Kijaji alisema kuwa dhana hiyo inatafsiriwa kwa kuangalia upatikanaji, ubora na gharama ya huduma za jamii zinazotolewa na Serikali.
Alisema baadhi ya huduma hizo ni pamoja na elimu, afya, maji, umeme na miundombinu ya usafiri na usafirishaji inayosaidia kupunguza gharama za usafirishaji wa bidhaa na na matengenezo ya vyombo vya usafiri.
Dhana nyingine ya kutafsiri ukuaji wa uchumi na maisha ya wananchi ni ushiriki wa wananchi wenyewe katika shughuli za kiuchumi hivyo ukuaji wa uchumi ni matokeo ya ushiriki wa wananchi katika uzalishaji mali na huduma.
Alisema kuwa wananchi wanaoshiriki katika shughuli za uchumi wananufaika kwa tafsiri ya dhana ya ukuaji wa uchumi kupitia huduma za kijamii zinazotolewa na Serikali pamoja na matokeo ya shughuli zinazofanywa na mwananchi.
Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kufanya jitihada za kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na biashara ili kila mtanzania aweze kutumia kikamilifu fursa zilizopo katika uzalishaji na huduma.
Naibu Waziri Dkt. Kijaji alisema kuwa uwekezaji katika viwanda utaongeza ajira na uzalishaji katika Sekta ya kilimo kwa kuwa Sekta hiyo inaajiri idadi kubwa ya watu nchini.
Social Plugin