Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TRA YAFAFANUA MABADILIKO YA SHERIA KWENYE VIWANGO VYA KODI

Na Veronica Kazimoto
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa ufafanuzi wa mabadiliko ya viwango vya kodi kama vilivyoainishwa na Sheria ya Fedha ya mwaka 2019 ambapo mabadiliko hayo yamegusa Sheria za Kodi ya Mapato, Ongezeko la Thamani (VAT), Usajili wa Vyombo vya Moto pamoja na Usalama Barabarani. 


Akizungumza wakati wa Wiki ya Elimu kwa Mlipakodi inayoendelea mkoani Morogoro katika Wilaya ya Mvomero, Afisa Msimamizi wa Kodi Mkuu wa TRA, Julius Mjenga amesema kuwa, mabadiliko katika sheria ya kodi ya mapato, jedwali la viwango vya kodi kwa wafanyabiashara wadogo wakazi, vimepunguzwa kutoka sh. 150,000 hadi kufikia sh. 100,000, kwa wale wenye mzunguko wa mauzo yanayozidi sh. milioni nne hadi milioni 7 kwa mwaka.

“Kwa wafanyabiashara wenye mauzo kati ya sh. milioni saba hadi sh. milioni 11, viwango vya kodi vimepunguzwa hadi kufikia sh. 250,000 kutoka sh. 318,000 iliyokuwepo hapo awali,” alisema Mjenga.

Pia, kwa wafanyabiashara wenye mauzo kati ya sh. milioni 11 hadi sh. milioni 14, viwango vya kodi vimepunguzwa hadi kufikia sh. 450,000 kutoka sh. 546,000.

“Lengo la kupunguza viwango hivi ni kukuza ridhaa ya kulipa kodi kwa hiari na kuongeza Mapato ya Serikali,” alifafanua Mjenga.

Kwa upande wa sheria ya usajili na uhamishaji wa umiliki wa vyombo ya moto, Mjenga ameeleza kuwa, ada ya kupata nakala ya kadi ya gari ni sh. 50,000, pikipiki ya magurudumu matatu (bajaji) sh.30,000 na pikipiki ni sh. 20,000 badala ya sh. 10,000 iliyokuwa ikitozwa kwa vyombo vya aina hiyo kabla ya tarehe 1 Julai, 2019.

Aidha, akizungumzia juu ya mabadiliko ya viwango vya leseni za udereva chini ya sheria ya usalama barabarani, Mjenga amesema kuwa, leseni ya udereva inalipiwa sh. 70,000 kila baada ya miaka mitano ambapo kabla ya mabadiliko ilikuwa inalipiwa sh. 40,000 kila baada ya miaka mitatu.

“Mabadiliko haya kwa ujumla wake yamelenga kuongeza fursa kwa walipakodi na wananchi kwa ujumla kuongeza ufanisi katika biashara zao na hatimaye kuongeza mapato ya Serikali. Hivyo, natoa rai kwa walipakodi wote kutumia fursa hii adhimu kwa maendeleo ya taifa letu,” alieleza Mjenga.

Wiki ya elimu kwa mlipakodi katika Mikoa ya Morogoro na Pwani itamalizika tarehe 17 Novemba, 2019 ambapo shughuli zinazofanyika ni pamoja na usajili wa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN), kupokea mrejesho, kusikiliza kero na kujibu maswali yanayoulizwa na wafanyabiashara pamoja na wananchi kwa ujumla.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com