MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, imefanikiwa kukusanya kiasi cha Tsh Trilioni 58.3/- ikilinganishwa makusanyo ya Tsh trilioni 34.97/- katika kipindi cha miaka minne iliyopita.
Hayo yamebainishwa leo (Jumatatu Novemba 25, 2019) Jijini Dar es Salaam na Naibu Kamishina Mkuu wa TRA, Msafiri Mbibo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa vyombo vya habari kuhusu mafanikio ya taasisi hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Mbibo alisema mwaka 2015/16, makusanyo ya mapato ya Mamlaka hiyo yalifikia Tsh trilioni 12.5/-, mwaka 2016/17 makusanyo yaliongezeka na kufikia Tsh Trilioni 14.4/-, mwaka 2017/18 makusanyo yaliongezeka pia hadi kufikia Tsh trilioni 15.5/- na mwaka 2018/19 makusanyo yaliongezeka zaidi na kufikia Tsh trilioni 15.9 na kufanya makusanyo yote ya jumla kufikia Tsh triloini 58.3/-.
‘Kwa miaka hii minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, TRA imekuwa ikikusanya wastani wa Tsh trilioni 1.3 kwa mwezi ikilinganishwa na wastani wa Tsh Bilioni 850/- kabla ya Awamu ya Tano haijaingia madarakani, sambamba na ongezeko hilo, kuanzia Julai hadi Oktoba 2019/2020 wastani wa makusanyo umepanda hadi kufikia Tsh trilioni 1.45/- kwa mwezi’’ alisema Mbimbo.
Aliongeza kuwa mafanikio hayo yametokana na msukumo wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kuendelea kuboresha mikakati ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato, kuibua vyanzo vya kodi pamoja na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Tano wa TRA wa ukusanyaji wa kodi wenye dhamira ya kuongeza makusanyo ya kodi za ndani kwa kukuza ulipaji kodi wa hiari.
Akifafanua zaidi Mbibo aliongeza kuwa sababu nyingine za kuongezeka kwa makusanyo hayo ni kuimarika kwa matumizi ya Mashine za Kielekroniki za Kutolea Risiti (EFD) badala ya stakabadhi zinazoandikwa kwa mkono, pamoja na kuboresha mifumo ya makusanyo inayoendana na mazingira ya sasa ya ukuaji wa sayansi na teknolojia.
Akizungumza kuhusu Mfumo wa Stempu za Kodi za Kielektoniki (ETS), Mbibo alisema mfumo huo ulioanza kutumika kuanzia Januari mwaka huu, umeiwezeha TRA kukusanya Tsh Bilioni 77.8/- uliotokana na ushuru wa bidhaa, kodi ya ongezeko la thamani na Kodi ya mapato yaliyokana na bidhaa za vileo, vinwaji baridi, maji, juisi na CD/DVD.
‘’Kutokana na utekelezaji wa mfumo huu kwenye eneo la pombe kali na mvinyo tu, TRA imekusanya ushuru wa bidhaa wa kiasi cha Tsh Bilioni 77.8/- kwa kipindi cha mwezi Februari hadi Oktoba 2019 sawa na ongezeko la Tsh Bilioni 19.6/- au ukuaji wa asilimia 34 ukilinganisha na kiasi cha Tsh Bilioni 58.2 kilichokusanywa kipindi kama hicho mwaka jana’’ alisema Mbibo.
Akibainisha mafanikio mengine, Mbibo alisema kufuatia mabadiliko ya Sheria ya Kodi na Mapato ya yaliyofanywa kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2019, Serikali imeweza kupunguza kiwango cha kodi kwa wafanyabiashara wadogo kutoka Tsh 150,000/- hadi kufikia Tsh 100,000/- kwa wale wenye mzunguko wa mauzo yanayozidi Tsh Milioni 4 kwa mwaka.
‘Kwa wafanyabiashara wadogo wenye mauzo kati ya Tsh Milioni 7- 12/- viwango vya kodi vimepunguzwa hadi kufikia Tsh 250,000/- kutoka Tsh 318,000/- wakati wafanyabiashara wenye mauzo kati ya Tsh Milioni 11- Milioni 14/- vinwango vya kodi vimepunguzwa hadi kufikia Tsh 450,000/- kutoka Tsh 546,000/-‘’ alisema Mbibo.
Mbibo alisema mafanikio mengine ya TRA ni kutangaza msamaha maalum wa riba na adhabu kwenye malimbiko ya madeni ya kodi kwa asilimia 100 tofauti na asilimia 50 ilivyokuwepo, ambapo lengo la msamaha huo ulitangazwa Julai mwaka 2018 ni kuwapa fursa walipakodi kulipa kodi ya msingi mara moja au kwa awamu ndani ya mwaka wa fedha 2018/19.
Anaongeza kuwa kutokana na hatua hiyo, jumla ya walipakodi 9,406 waliomba msamaha na waliokidhi vigezo na kukubakliwa ni walipakodi 8687, ambapo jumla ya Tsh Bilioni 328.4 za riba na adhabu zilisamehewa wakati jumla ya Tsh Bilioni 458.58 zinaendelea kukusanywa kama kodi ya msingi.
‘’Mpaka sasa, Mamlaka imeshakusanya Tsh. Bilioni 120.01 kutokana na kodi ya msingi inayotakiwa kulipwa na walipakodi waliosamehewa riba na adhabu, pia Serikali iliongeza muda uliowekwa awali wa Juni 30, 2019 kuwa Desemba 31, 2019’’ alisema Mbibo.