Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Murilo
Mwanaume mmoja amefariki dunia na wengine kumi na moja kujeruhiwa baada ya kugongwa na gari lililoacha njia na kuwagonga wakiwa pembezoni mwa barabara ya Furahisha eneo la Mkunguni Jijini Mwanza.
Tukio hilo limetokea majira ya saa 10:30 Alfajiri ambapo gari lenye namba za usajili T 946 DPL TOYOTA Crawn kuacha njia na kuwagonga wafanyabiashara ndogondogo pamoja na watembea kwa miguu waliokuwa wakitoka kanisani kwenye mkesha wa Krismasi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Murilo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na tayari dereva wa gari, Desisi Omary (29) anashikiliwa na Jeshi la Polisi huku akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoani humo.
"Tukio hilo limetokea barabara ya Furahisha, lililopo eneo la Mkunguni ambapo gari hilo liliwagonga wafanyabiashara ndogondogo pamoja na watembea kwa miguu waliokuwa wakitoka kanisani na kusababisha kifo cha mtu mmoja ambaye mpaka sasa bado hatujajua utambulisho wake", amesema Kamanda Murilo.
Kwa upande wake Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Sekou Toure amesema wamepokea jumla ya watu 11, mmoja kati yao akiwa ameshafariki na wengine 10 wakiwa majeruhi huku watano wakihamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Bungando.