Bodi ya wanafunzi wa elimu ya juu (HESLB) nchini Tanzania inakamilisha malipo ya wanafunzi waliobadilisha kozi waliyoyapokea kutoka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ambazo zitawafikia kuanzia kesho Jumatano Desemba 18, 2019.
Taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul- Razaq Badru iliyotolewa jana Jumatatu Desemba 16, 2019 ilizungumzia malalamiko yaliyotolewa na wanafunzi wa vyuo mbalimbali, kikiwamo Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM).
“Kuna kundi la wanafunzi waliobadilisha kozi wakiwa vyuoni na taarifa hizo zilikua hazijatufikia, tumezipokea mwishoni mwa wiki na tunakamilisha malipo ambayo yatawafikia siku mbili zijazo,” alisema Badru
Alisema kundi jingine linahusu malipo ya vitabu na viandikwa, ambapo malipo ya awamu ya kwanza ya jumla ya Sh13.3 bilioni yameshafanyika na awamu ya pili ya Sh1.1 bilioni itawafikia wanafunzi ifikapo Jumamosi ijayo, Desemba 21, 2019 kwa kuwa wataalamu wao wanakamilisha uchambuzi.
Badru alisema hadi sasa, wanafunzi 49,485 wa mwaka wa kwanza wameshapata mikopo yenye thamani ya Sh169.4 bilioni na kuvuka lengo la kutoa mikopo kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza wapatao 45,000.
Social Plugin