Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti
Na Ashura Jumapili - Malunde 1 blog
MKUU wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti,amesema hataki kusikia suala la upungufu wa madarasa na kuzitaka halmashauri zote za Wilaya mkoani humo kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu wanapokelewa na kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2020.
Brigedia Jen.Gaguti,alitoa agizo hilo katika kikao cha wadau wa elimu mkoani humo kilichofanyika katika Manispaa ya Bukoba.
“Wanafunzi wote waliofaulu wapokelewe kwenye shule walizopangiwa kwa wakati kwaajili ya kuanza masomo yao ya kidato cha kwanza”alisema BrigediaJen.Gaguti.
Awali Ofisa elimu mkoa wa Kagera Juma Mhina,alisema kuwa mkoa wa Kagera una kabiliwa na upungu wa vyumba vya madarasa 283.
Mhina ,alisema halmashauri zinahimizwa kushirikisha jamii na wadau mbalimbali wa elimu katika ujenzi wa vyumba vya madarasa na utengenezaji wa madawati ili ifikapo mwezi Machi ,2020 wanafunzi waliofaulu waweze kujiunga na kidato cha kwanza.
Alisema Wilaya inayoongoza kwa upungufu wa vyumba vya madarasa ni Wilaya ya Muleba vyumba 66,Karagwe vyumba 56,Biharamulo vyumba 37,Kyerwa 32,Bukoba Manispaa 32,halmashauri ya Bukoba 32,Missenyi 31 na Ngara vyumba 8.
Mwalimu Aidan Bahama,ni mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Ngara ,alisema jitihada za kupunguza uhaba wa vyumba vya madarasa zilizotokana na kikao cha wadau wa elimu cha mwaka 2018 wilayani humo.
Bahama,alisema Wilaya ya Ngara mwaka jana ilikuwa na upungufu wa vyumba saba vya madarasa .
“Tuliona kuna upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa kwa shule za sekondari na msingi ,Wilaya ilifanya tathimin kuona shule zenye upungufu na idadi ya madarasa yanayohitajika kwa shule husika”alisema mkurugenzi.
Alisema baada ya tathimini mkurugenzi na mkuu wa Wilaya ya Ngara walishirikiana wakaamua kujenga vyumba Zaidi ya vilivyokuwa vinahitajika hivyo walijenga vyumba 22 badala ya vyumba 7.
Alisema Rais kupitia kwa Wazairi wa Tamisemi alitoa kiasi cha shilingi milioni 25 kwa kila shule ambazo zilisaidia kukamilisha maboma yaliyokuwa hayajakamilika na kuongeza vyumba vingine na kuwa na jumla ya vyumba 48 vya madarasa.
Alisema hata huo upungufu wa vyumba vya madarasa 8 mwaka huu vipo katika hatua mbalimbali za ukamilishaji hadi kufika mwezi Januari 2020 hakutakuwa na upungufu wa chumba hata kimoja.
Alisema mafanikio hayo ni nguvu ya pamoja kati ya mkurugenzi,mkuu wa wilaya,wananchi na wadau wa elimu wilayani ngara.
Mwisho.