Na Veronica Kazimoto, Dar es Salaam
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), inatarajia kuanzisha Kampeni ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi katika Mkoa wa Dar es Salaam itakayodumu kwa siku 13 kuanzia kesho tarehe 2 hadi 14 Desemba, 2019.
Akizungumzia kampeni hiyo leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo amesema kuwa lengo ni kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali ya kodi pamoja na kusikiliza malalamiko, changamoto na kupokea maoni kutoka kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla.
"Kampeni hii ni mwendelezo wa kampeni ambayo imemalizika katika Mikoa ya Morogoro na Pwani na sasa tunaingia katika Mkoa wa Dar es Salaam tukiwa na lengo la kuwaelimisha walipakodi na wananchi masuala yanayohusu kodi, kupokea maoni yao, kusikiliza changamoto na malalamiko ili tuweze kuyatafutia ufumbuzi", alisema Kayombo.
Kayombo ameongeza kuwa kampeni hiyo itaambatana na huduma ya usajili wa wafanyabiashara wapya wasiokuwa na Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi yaani TIN.
"Pamoja na kutoa elimu ya kodi, kupokea maoni na kusikiliza changamoto za walipakodi pia tutatoa huduma ya usajili wa walipakodi wapya ambapo tutawapatia cheti cha Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi tukiwa na dhumuni la kupanua wigo wa walipakodi hapa nchini", aliongeza Kayombo.
Mkurugenzi Kayombo amebainisha maeneo ambayo yatafikiwa katika kampeni hiyo kuwa ni Ilala, Kinondoni, Temeke na Kariakoo na itafanyika kwa njia ya semina katika vituo vilivyopangwa kwenye maeneo hayo pamoja na kuwatembelea walipakodi katika biashara zao yaani duka kwa duka.
MWISHO.
Social Plugin