Dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi
Mwanamke mmoja katika wilaya ya Hoima Mashariki mwa Uganda anashikiliwa kwa madai ya kumuua mpenzi wake baada ya kumfuma akimeza dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi (ARV).
Polisi wamesema siku ya Alhamisi kuwa Emmanuel Tumusiime, 35 alishambuliwa mpaka kuuawa katika makazi yake akiwa mji wa Kigorobya majira ya saa kumi na mbili jioni siku ya Jumatano.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor nchini Uganda, msemaji wa polisi wa mji huo, Bwana Julius Hakiza amesema uchunguzi wa awali ulibaini kuwa Tumusiime alipigwa kichwani na shoka.
''Alipogundua kwamba mpenzi wake amefariki, mshukiwa alifunga nyumba na kupanda Bodaboda mpaka kwenye kituo kikuu cha polisi cha Hoima na kuripoti kesi ya mauaji,'' alieleza Bw. Hakiza.
Katika kituo hicho cha polisi, mwanamke huyo alikiri kumuua mpenzi wake.
Mwanamke huyo anadai kuwa alijisikia uchungu sana baada ya kuhisi kuwa kuna uwezekano ameambukizwa virusi vya Ukimwi.
Alikamatwa na kushikiliwa kwenye kituo kikubwa cha Hoima akishutumiwa kwa kujihusisha na mauaji.
Wapelelezi walikimbilia eneo la tukio na kulifunga kwa ajili ya uchunguzi zaidi, alieleza Hakiza.
''Tunatoa wito kwa waathirika wa virusi vya Ukimwi mara zote kuwapa taarifa wenza wao na kuhudhuria vituo vya ushauri nasaha na kufahamu kwamba kwa kuwa mwathirika, haimaanishi ni mwisho wa maisha,'' alishauri Hakiza.
Chanzo -BBC
Social Plugin