Waokoaji nchini Kenya wameuopoa mwili wa kijana mmoja aliyekufa maji alipokuwa akijaribu kumuokoa mwananume ambaye alikuwa akiomba usaidizi alipokuwa akivuka mto uliokuwa umefurika.
Anna Nduku mwenye umri wa miaka 19 alianguka katika mto Kandisi karibu na eneo la Ongata Rongai , viungani vya mji mkuu wa Nairobi siku ya Jumanne.
Ni miongoni mwa zaidi ya watu 130 ambao wamefariki kutokana na mafuriko yanayosababishwa na mvua kubwa ambayo imekuwa ikinyesha tangu siku ya Jumanne.
Bi Nduku alikuwa akijibu kilio cha mwanaume aliyekuwa akining'inia katika eneo moja la daraja ambalo liikuwa likijengwa.
Mwanaume huyo aliokolewa lakini yeye akaanguka katika mto huo alipojaribu kumuokoa.
Mamake Nduku, Elizabeth Mutuku, alikuwa karibu wakati ajali hiyo ilipotokea.
''Nilimuona akijaribu kujitoa katika maji nikajaribu kumuokoa. Nilimwita Anna Anna! Nilitaka kumrushia kijiti ili kujaribu kumvuta lakini mto huo ulikuwa umejaa maji hivyo basi alikuwa akirushwa kutoka eneo moja hadi jingine kabla ya kusombwa na maji hayo''.
Mto huo ulikuwa umefurika kutokana na mvua kubwa inayonyesha ambayo ilianza siku ya Jumatatu.
Ni baadhi ya mvua zilizoripotiwa katika eneo la Afrika mashariki katika wiki za hivi karibuni.
Wakazi wanasema kwamba hii ni miongoni mwa ajali za hivi karibuni ambazo zimefanya watu kadhaa kusombwa na maji katika kipindi cha miaka miwili iliopita.
Daraja la zamani liliondolewa mwaka 2017 na daraja jipya bado halijakamilishwa. Hatua hiyo imewafanya wakaazi kupitia maji kwa kutumia mawe wanayokanyaga ili kuvuka mto huo.
Dada yake Nduku , Maryam Zenneth, amelaumu serikali za mitaa kwa kushindwa kumaliza daraja hilo ambalo ni kiunganishi muhimu kati ya kijiji chake na mji wa soko wa Ongata Rongai.
''Watu wengi wanafariki na wao wanatazama watu wakiendelea kupoteza maisha'' , aliiambia BBC huku akiwa amejawa na hasira.
''Wanakuja na kuomboleza nawe lakini hawachukui hatua yoyote, leo ni dada yangu kesho atakuwa nani''?
''Daraja hilo ndio barabara kuu miongoni mwa watoto wanaokwenda shule. Kwa nini waliliondoa daraja lililokuwepo ili kuanza kujenga jipya na hawalimalizi kulijenga''?Watu hupanda katika daraja hilo ambalo halijakamilisha ili kujaribu kuvuka mto huo
Serikali ya mitaa katika eneo hilo bado haijatoa tamko lolote . Akikumbuka kuhusu maisha ya mwanawe, mamake amesalia akiwa amevunjika moyo. 'Nina huzuni, pengine angekuwa kiongozi wa siku zijazo ama hata mwalimu. Kupoteza maisha kama hayo kutokana na daraja ni uchungu mwingi."
Mvua zaidi inatarajiwa kunyesha katika taifa hilo katika siku zijazo , na serikali inawashauri watu wanaoishi katika maeneo ambayo yametabiriwa kuathiriwa vibaya kuhamia katika maeneo salama.
Maeneo mengine katika eneo hilo , watu sita wamefariki mashariki mwa Uganda kufuatia maporomoko ya ardhi baada ya mvua kunyesha kwa siku mbili mfululizo na kufikia sasa takriban watu 50 hawajulikani waliko.
Social Plugin