Na Sharon Sauwa, Mwananchi
Mkurugenzi wa kampuni ya Scol Building Contractors Limited ameanguka na kuzirai mbele ya Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo baada ya kubanwa kuhusu ucheleweshaji wa ujenzi wa barabara ya Martin Luther hadi Swaswa mjini Dodoma.
Tukio hilo limetokea leo Jumatano Desemba 4, 2019 baada ya Jafo kutembelea ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita nane iliyotakiwa kukamilika Agosti lakini ukaongezwa muda hadi Oktoba, 2019. Alizirai baada ya kuelezwa na Jafo kuwa kusuasua kwake kutasababisha asipewe kazi nyingine za ujenzi wa barabara.
Kutokana na kuchelewa huko mkandarasi huyo amekatwa Sh80 milioni na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura).
Licha ya kujitetea kuwa wamejenga katika miradi mingi nchini ikiwemo katika jimbo la Kisarawe ambalo mbunge wake ni waziri huyo wa Tamisemi, waziri huyo alikataa na kubainisha kuwa uwezo wa kampuni hiyo ni mdogo.
Baada ya hoja hiyo kupanguliwa na Jafo, mkurugenzi huyo alijitetea kuwa anakwamishwa na upatikanaji wa malighafi.
“Si watu wengi wanaweza kutumia hii nyenzo, hili jiwe hili linatoka Lugoba, Sisi tunataka tufanye kazi nzuri,” alijitetea mkurugenzi huyo.
“Umeshatembelea kazi za wenzako ukafanya ulinganisho ,” amehoji Jafo na huku mkurugenzi huyo akikosa jibu.
Hali hiyo ilimfanya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge kusema inawezekana kuna kinachomfanya kuchelewesha kazi, ndio maana anashindwa kusema ukweli.
“Katika sehemu ambayo sina shaka na mkurugenzi wangu, mhandisi wa Mkoa wa Dodoma wala mkuu wangu wa Mkoa ni eneo hili la usimamizi wa miradi kwa sababu miradi inaenda vizuri sana,” amesema Jafo.
Jafo amesema katika mradi huo changamoto ipo kwa mkandarasi, akibainisha kuwa Dodoma wamejenga barabara nyingi zimekamilika katika muda mfupi.
“Injinia kuna miradi mingine mmempatia hapa Dodoma,” amehoji Jafo na kujibiwa kuwa hakuna miradi mingine aliyopewa.
Alitoa agizo kwa viongozi wa Dodoma kutompatia mradi mwingine mkandarasi huyo huku akitilia shaka kasi yake ndogo na ubora wa barabara.
Jafo aliagiza mkandarasi huyo kuendelea kukatwa fedha hadi kazi itakapokamilika, kwamba ujenzi wa barabara hiyo unatakiwa kukamilika Desemba 30, 2019.
“Hizo blablaa zako za kokoto zinatoka mbali na nini sitaki kuzisikia, wenzako wote wanatengeneza barabara wanatoa wapi. Labda huna mtaji. Wakazi wa hapa wameteseka sana na madimbwi ndio maana tukasema tuunganishe hii barabara,” amesema Jafo.
Waziri huyo amesema ikiwa mradi huo hautakamilika Desemba 30 atawapiga marufuku wataalam wake wote kumpa kazi nchini.
“Wewe unakuja hapa ndio injinia ama mkurugenzi mbona sikuelewi. Ikifika tarehe 30 kazi hii isipokamilika hamtapata kazi yoyote nchini,” amesema Jafo na ghafla mkurugenzi huyo akaishiwa nguvu na kuanguka na Jafo kumtaka asimame na kusisitiza kuhusu Serikali kutotaka kufanya kazi na Mkandarasi mbabaishaji.
Chanzo - Mwananchi
Social Plugin