Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Tano Mwera
Na Andrew Chale - Busega
TAMASHA kubwa la kuibua na kukuza Utalii ndani ya Wilaya ya Busega la 'Lamadi Utalii Festival' linatarajiwa kufanyika kwa siku nne ndani ya viwanja vya shule ya msingi Itongo, Lamadi kuanzia Desemba 29 hadi Januari mosi 2020.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kamati wa tamasha hilo lenye kauli mbiu "Utalii wa Ndani Unawezekana" Mkuu wa Wilaya ya Busega Bi. Tano Mwera amesema tayari asilimia kubwa maandalizi yanaendelea vizuri huku akitoa wito kwa wadau kujitokeza kwa wingi.
"Watu wote tunawakaribisha kujitokeza kulishuhudia tamasha kubwa la Utalii Lamadi.
Kila mtu atalishuhudia bure na hakuna kiingilio kwani tumedhamilia kutoa fursa za kibiashara na kukuza uchumi shime tuje kwa wingi katika mji wa Lamadi kuona vivutio vya Utalii, Malikale, Maliasili, Utamaduni na vingine vingi ikiwemo vikundi vya ngoma na bidhaa mbalimbali zitauzwa" alisema Mkuu wa wilaya Bi. Tano Mwera.
Aidha, ametoa wito kwa Wajasiliamali na wadau wa biashara kuchangamkia fursa za kibiashara
"Siku zimebaki chache. Nachukua nafasi hii kuwakaribisha wajasiliamali wote kutoka Busega, Kutoka Wilaya zingine za Mkoa wa Simiyu na mikoa jirani kuja kuuza bidhaa zao tamasha letu fursa kemkem" alieleza Bi. Tano Mwera.
Pia ametoa wito kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi 'Diaspora' na wadau wengine kutumia likizo ya mwishoni mwa mwaka kufika Lamadi kujionea utajili wa Utalii ilipo pamoja na ule wa eneo jirani na mji huo.
"Mji wa Lamadi upo shwari. Tumejiandaa kupokea wageni kutoka kona zote. Suala la malazi na usalama wa raia na mali zao kwa kipindi chote" alisema Bi. Tano Mwera.
Tayari kamati ya maandalizi na wadua wamekutana kuhakikisha wanafanikisha tamasha hilo.
"Nimeshakutana na wadau wa kamati zangu kuhakikisha tunafanya kitu kikubwa. Wadau hao ni: Mkurugenzi Kisesa Cultural Group Nelson Machibya, Afisa Utalii Jiji la Mwanza Sifuni Sospatery,
Mkuu wa Kanda Idara ya Utalii, John Semkubay.
Wengine ni Afisa Utalii kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Victor Bundala, Mkuu wa Bodi ya Utalii Kanda Ya Ziwa Gloria Munhambo, Muhifadhi Mkuu Kisiwa Cha Saanane, Eva Mallya, Meneja wa pori la Akiba Kijereshi, Diana Chambi na Mwakilishi kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA)." Alimalizia Bi. Tano Mwera.
Miongoni mwa vitu vitakavyopatikana kwenye tamasha hilo ni pamoja na vitu hivyo vya Asili, wachora picha za tingatinga, wasusi wa nywele, mikeka, wachonga vinyago, vyakula vya asili, nyama choma, uchomaji wa samaki (Sato corner ) na mengine mengi.
Kwa mwaka huu tamasha hilo linatarajiwa kuwa la kwanza ambapo lilihasisiwa na kuzinduliwa rasmi Oktoba 23 mwaka huu siku ya Baraza la Biashara na Uchumi Wilayani Busega.