RAIS MAGUFULI AONGOZA WATANZANIA KATIKA MAPOKEZI YA NDEGE YA BOMBARDIER Q400 JIJINI MWANZA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli, ameongoza watanzania katika mapokezi ya ndege ya Bombardier Q400 jijini Mwanza leo Desemba 14, 2019.


Katika hotuba yake Rais Magufuli ameeleza safari nzima ya ndege hiyo kutoka Canada hadi kufika Tanzania.

'Ndege yetu ya Bombardier Q400, imetoka Canada jana, imepita Iceland, Czech Republic, ikatua Misri na leo imeondoka Misri ikatua Addis Ababa Ethiopia na sasa ipo njiani kuja hapa itafika kwenye saa 1:00 au saa 2:00 hivi usiku huu' - Rais Magufuli.

Aidha amefafanua manunuzi ya jumla ya ndege 11 kwa kusema, 'Tumenunua jumla ya ndege 11 na hii inayokuja leo ni ya 8 hivyo bado tatu, ambapo mwakani tena mwezi Juni tutapokea Bombardier Q400 nyingine itatua nchini'.

Aidha amebainisha uwepo wa safari ya ndege ya moja kwa moja kutoka Mwanza hadi London. 'Nimeongea na Rais Kagame wa Rwanda ana mpango wa ndege moja iwe inatoka Kigali kuja Mwanza kisha kutoka Mwanza moja kwa moja kwenda London'.

Mbali na hayo Rais Magufuli akatoa ofa ya kupanda bure kwa wajumbe wa NEC CCM pamoja na wengine wanaosafiri kwenda Dar es salaam.

'Kesho saa 3:00 Asubuhi wajumbe wa NEC CCM wapande bure kwenda Dar es salaam na Zanzibar na wengine wote wanaotaka kusafiri kwenda huko' - Amesema Rais Magufuli.

Pia ameagiza marubani wanaokuja na ndege hiyo wapewe zawadi, 'Vijana wetu wanaokuja na ndege hii, naomba muwaandalie angalau milioni 2 kila mmoja kama motisha ya uzalendo wao na kujitoa kwa taifa' - Rais Magufuli.

Mwisho Rais amewapongeza wafanyakazi wote wa ATCL na kuwataka wawapuze watu wanaowabeza. 'Wafanyakazi wa Air Tanzania chapeni kazi, watatokea tu watu wa kuwakosoa. Eti mlivyo wazuri hivi mnavaa vizuri mtu anasema ni wabaya, nyie chapeni kazi na nawapongeza sana' - Rais Magufuli.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post