Na; Salvatory Cevin
Baada ya kukithiri kwa matukio ya wanafunzi kupata mimba na uwepo wa ndoa za watoto chini ya umri wa miaka 18 mkoani Shinyanga, hatimaye serikali imeamua kutoa fomu maalum ambazo zitasaidia kuzihakiki ndoa zote zinazotarajiwakufungwa.
Hayo yamebainishwa juzi na Ofisa maendeleo ya jamii wa mkoa wa Shinyanga, Tedson Ngwale katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa watoto na wanawake yaliyofanyika katika kijiji cha Penzi kata ya Mondo wilayani Kahama yaliyofadhiliwa na shirika la World Vision.
Amesema katika mkoa wa Shinyanga kila halmashauri itapewa fomu hizo maalum ambazo zitatumika kama mkataba wa kuhakiki ndoa zote katika maeneo yote baada ya kubaini ndoa nyingi zinazofungwa ni za wanafunzi pamoja na watoto chini ya umri wa miaka 18.
“Fomu hizi zitahitaji mwoaji awasilishe nyaraka mbalimbali ili kutibitisha umri wa anayekwenda kuolewa kama vile vyeti vya kuzaliwa kutokana na kuwepo kwa ndoa batili za watoto ambazo zinafanyika kwa siri hususani katika maeneo ya vijijini”alisema Ngwale.
Ngwale amesema watendaji wa vijiji na kata watapaswa kufanya uhakiki huo kwa kina kabla ya kuruhusu kufanyika kwa ndoa hizi kwa kutumia fomu hizo ambazo zitakuwa na kiapo maalum ambacho kimtaka kuijaza kwa uaminifu na uadilifu.
Mbali na hilo, Ngwale amesema Serikali imeandaa mikataba maalum baina ya wazazi wa wanafunzi baada ya kubaini wazazi mkoani humo kuwazuia watoto wao wakike kufanya vizuri katika masomo yao ili waolewe jambo ambalo ni kinyume na haki za watoto.
“Katika mitihani ya mwisho hususani wa darasa la saba watoto wengi wakike katika baadhi ya jamii mkoani humu wamekuwa wakizuiwa kufanya vizuri ,kupitia mikataba hii suala hili litakuwa limefikia mwisho kwani mwanafunzi akibainika kufanya vibaya wazazi watakuwa wanachukuliwa hatua za kisheria”alisema Ngwale.
Kwa upande wake Ofisa mradi wa ENRICH kutoka shirika la World vision, Magreth Mambali amesema katika siku hizi 16 za kupinga ukatili wa kijinsia wamebaini katika maeneo ya vijijini wanawake na watoto ndio wahanga wa ukatili.
“Mila na tamaduni za kabila la wasukumu bado ni kandamizi kwa wanawake hususani watoto wakike kwani husababisha wengi wao kuolewa katika umri mdogo na kukosa haki zao za msingi kama vile elimu”alisema Mambali.
Takwimu za mimba kwa wanafunzi kwa mwaka 2018 katika mkoa wa shinyanga zinaonesha wanafunzi 69 walipata mimba huku mwaka huu wa 2019 wanafunzi waliopata mimba wakiwa ni 120.
Mwisho.
Social Plugin