Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limethibitisha kumshikilia mtu mmoja aliyetambulika kwa jina la Benson Bernard Sadala Shila (31) mkazi wa Kihonda, Manispaa ya Morogoro, ambaye ni fundi Welding baada ya kukutwa uchi mtoni na mtoto wake aitwaye Goodchance Bernard (7), ambaye anasoma darasa la awali katika Shule ya Ebeneza mjini humo, huku akiwa na panga na msumeno akitaka kumdhuru mtoto huyo.
Hayo yamesemwa leo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Hamis Issah ambaye ameeleza kuwa tukio hilo lilitokea juzi Alhamisi, Desemba 19, 2019, katika eneo la Maporomoko ya Mlimani Nguzo Camp, Kata ya Boma, Manispaa ya Morogoro ambapo wasamaria wema walimtilia mashaka waliposikia mtoto akisema “baba unaniua”, waliwaita polisi haraka.
Amesema baada ya kufika eneo la tukio, askari walimtaka mtuhumiwa huyo atoke kwenye maji, lakini alikataa na kuendelea kutoa lugha zisizoeleweka kwa askari kisha kujirusha kwenye maporomoko hayo makali ya maji. Askari shupavu na wenye weledi, waliamua kujitosa kwenye maji na kumwokoa mtu huyo na mtoto. Pembeni palikutwa panga na kipande cha msumeno.
“Akiwa na nguvu za ajabu alitaka kujizamisha kwenye maji pamoja na mtoto huyo huku akitamka maneno yasiyoelekwa na kwa hisia kali. Walimdhibiti na kumtoa kwenye maji na kumpa huduma ya kwanza kabla ya kumfikisha katika Kituo Kikuu cha Polisi Morogoro.
Mtoto huyo alikabidhiwa kwa mama yake, lakini mtuhumiwa anaendelea kushikiliwa kwa uchunguzi zaidi, na tunashirikiana na wenzetu wa hospitali (matabibu) ili kupima afya yake ya akili na tutatoa ripoti kamili,” amesema Kamanda Issah.
Kwa upande wake mke wa mwanaume huyo, Marry Shao amesema kuwa yeye na mumewe wana watoto wawili .
"Mume wangu alianza kubadilika Novemba 29, 2019 siku ijumaa, kwakweli alianza kuongea mambo ambayo mimi siyaelewi, alikuwa anaongea mambo ya ufalme wa mbinguni, na siku ya tukio alikuwa yuko tu vizuri hadi anaondoka na mtoto alikuwa sawa" amesema Marry.
Social Plugin