Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi linamshikilia ofisa muuguzi msaidizi wa kituo cha afya Mamba Wilaya ya Mlele, Abednego Nkona (32) kwa tuhuma za kumbaka mjamzito wakati akijifungua.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi,Benjamin Kuzaga alisema tukio hilo la kinyama na la kikatili lilitokea Desemba 18, mwaka huu saa 2 usiku katika chumba cha kujifungulia wajawazito.
Alisema siku ya tukio, mwanamke huyo alipatwa na uchungu wa kujifungua baada ya siku zake kutimia, alitoka nyumbani kwake Majimoto kwenda kupata huduma kituoni hapo, huku akisindikizwa na mama yake mzazi.
Baada ya kufika kituoni alipokelewa na Alfred ambaye alikuwa muuguzi wa zamu siku hiyo.
Alisema muuguzi alianza kumpatia huduma ya uzazi, lakini mwathirika wa tukio hilo alihisi hali isiyo ya kawaida sehemu zake za siri hali ambayo ilimfanya ashituke.
Alisema baada ya kubaini hilo na kuingiliwa licha ya kuwa hatua za mwisho kujifungua alipiga kelele.
Alisema baada kuona hivyo, mjamzito aliamua kuinuka kitandani na kwenda moja kwa moja kutoa taarifa kwa mama yake mzazi, Mektilida Deogratius ambaye alitoa taarifa kwa uongozi wa kituo.
Mtuhumiwa baada ya kufanya kitendo hicho, alitokomea kusikojulikana, lakini polisi walifanikiwa kumkamata.
Kamanda Kuzaga, alisema mtuhumiwa anaendelea kushikiliwa na anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote ili akajibu tuhuma hizo.
Social Plugin