TAKUKURU Mkoani Dodoma wanamshikilia Mkuu wa Shule ya Sekondari Serengeti iliyopo Serengeti Mkoani Mara, Baraka Sabi kwa tuhuma za kuomba rushwa ya ngono kwa Mwanafunzi aliyemaliza kidato cha sita katika shule hiyo ili ampatie cheti chake cha kuhitimu.
Akiongea na Waandishi wa Habari leo Jumapili, Kamanda Wa Takukuru Mkoa wa Dodoma Sosthenes Kibwengo amesema wamemkamata Mkuu huyo wa shule kwa kushirikiana na Mwanafunzi aliyeombwa rushwa ya ngono Mkazi wa Dodoma ambaye alihitimu mwaka 2016 na alikuwa anataka cheti aombee kazi
“Mwalimu Baraka alimwambia Mwanafunzi asipate shida ya kwenda Serengeti yeye ana safari ya kuja Dodoma katika Mkutano wa Wakuu wa Shule na atakuja na cheti, walipokutana akaomba rushwa ya ngono ndipo ampe cheti, Msichana akaomba udhuru na kuahidi kurejea, kisha akatutonya” -Amesema Kibwengo
Amesema baada ya kupokea taarifa hiyo waliweka mtego na kufanikiwa kumkamata akiwa na mtoa taarifa kabla yakufanya tendo hilo.
Amesema Takukuru walifanikiwa kuchukua cheti hicho na uchunguzi wa awali unaendelea kwa mujibu wa sheria na hatua stahiki zitachukuliwa baada ya kukamilika.
Social Plugin