Polisi eneo la Suna Magharibi, kaunti ya Migori nchini Kenya wanamsaka mwanamke mwenye umri wa makamo aliyetoweka baada ya kumdunga kisu shemeji yake.
Eunice Adhiambo alitekeleza kisa hicho baada ya mabishano makali kuzuka baina yake na shemejiye mnamo Jumanne, Disemba 24,2019.
Kulingana na chifu wa eneo hilo Yogo Tumbo, marehemu alikuwa amemtembelea mshukiwa ambaye alimkuta akimenya mihogo kulingana na ripoti ya Citizen TV.
Inadaiwa, jamaa aliyejaribu kujadiliana kuhusu jambo fulani ambalo bado halijajulikana alimzaba kofi Eunice katika makalio yake baada ya kuhisi mshukiwa alikuwa akimpuuza.
Punde si punde, mshukiwa anadaiwa kumrukia marehemu na kumdunga kisu mara kadhaa kifuani akitumia kisu alichokuwa nacho mkononi.
Chifu huyo alidokeza kwamba, marehemu alifariki papo hapo na mwili wake umehifadhiwa katika makafani ya hospitali ya Migori Level Four ukisubiri upasuaji.
Social Plugin