WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA AFANYA ZIARA KWENYE KIWANDA CHA NGUO CHA MWATEX MWANZA


Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa, amefanya ziara katika kiwanda cha Mwatex (2001) LTD kilichopo mkoani Mwanza leo. Kiwanda hicho ambacho kilibinafsishwa na Serikali na kupewa mwekezaji Amin Radhanin kimeajiri wafanyakazi zaidi ya 600 na kinaendelea na uzalishaji kwa asilimia 60 kutokana na changamoto mbalimbali.

Aidha katika ziara yake Mhe. Bashungwa alizungumza na uongozi wa kiwanda na pia kusikiliza kero za wafanyakazi, ambapo wafanyakazi walipata fursa ya kumueleza Waziri changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Mtumishi wa kiwanda hicho aliyetambulika kwa jina la Thomas Mashauri alieleza kuwa kuna rushwa katika masuala ya ajira, na kueleza kwamba ili uweze kuajiriwa ni lazima utoe hongo ya kiasi cha shilingi elfu hamsini (50,000) ndipo uajiriwe. Aidha aliongeza kusema kuwa wafanyakazi wanalazimishwa kufanya kazi kwa kutumia mashine mbili kwa wakati mmoja pasipo kuangalia jinsi gani mfanyakazi anaumia.
Ndugu Mashauri aliongeza kuwa wasimamizi katika kiwanda hicho hawana kauli nzuri kwa wafanyakazi na pia wamekuwa wakali.

Pia wafanyakazi wa kiwanda cha MWATEX walieleza changamoto ya upatikanaji wa vipuli (spare parts) vya mashine mbalimbali katika kiwanda hicho inayopelekea mashine nyingingi kutokufanya kazi na muda mwingi kutumika kwa ajili ya matengenezo.

Baada ya kusikiliza kero za wafanyakazi na kuona utendaji wa kiwanda usioridhisha Mhe. Bashungwa ameagiza Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, TIRDO, Dar Tech, VETA, SIDO, NDC kuunda kamati maalumu ambayo itatembelea kiwanda hiki na kufanya uchambuzi wa uendeshaji wa kiwanda kwa kushirikiana na msimamizi wa kiwanda.

Mhe. Bashungwa ametoa muda kuchunguza mwenendo wa kiwanda hiki hadi kufikia tarehe 1/1/2020 kamati husika iwe imekamilisha kazi na kukabidhi ripoti yake kwa Waziri.
Aidha Mhe. Bashungwa amesema kwamba ripoti husika itasaidia Serikali katika kutatua changamoto zinazokabili kiwanda hiki ili kiendelee kuzalisha kwa asilimia 100 kama ilivyo mkakati wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kuhakikisha viwanda vyote vilivyobinafsishwa vinafufuliwa, vinafanya kazi na kuongeza uzalishaji kwa asilimia 100, ili kutengeneza mnyororo wa thamani ya mazao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post