Naibu Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara Mhe.Stella Martin Manyanya(Mb) amewataka wawekezaji kutoka Kituo cha Biashara cha Slovakia,Afrika na Uarabuni(SAAOK) kufanya uwekezaji utakao kuwa na manufaa kwa wazalishaji wa bidhaa za Viwanda nchini.
Akizungumza na Watendaji wa Kituo hicho tarehe 20 Desemba,2019 Jijini Dar es Salaam kwenye kikao kilicholenga kuwaelezea fursa za uwekezaji zinazopatika hapa nchini Mhe.Manyanya amesema bado Tanzania inahitaji wawekezaji kwenye sekta ya mifugo ili kuboresha bidhaa za ngozi.
"Tanzania ina ng'ombe milioni 50,ni idadi kubwa lakini ufugaji wake sio wa kuzingatia ubora wa malighafi zinazohitajika kuzalisha bidhaa za ngozi zenye kiwango cha kimataifa.Kwahiyo uwekezaji kwenye sekta ya mifugo utahakikisha upatikanaji wa malighafi zenye ubora wa kimataifa kwa ajili ya Viwanda vya bidhaa za ngozi"
Pia amewataka kuwekeza kwenye Viwanda vya kutengeneza mashine zikazowasaidia wakulima kuongeza uzalishaji na kusaidia uchakataji malighafi ili kuziongezea thamani.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa SAAOK Bw.Zine Laroussi amesema kituo hicho kinafanya miradi mbalimbali kwenye nchi zinazoendelea ikiwa ni pamoja na Nishati,Maji,Chakula,Elimu,Usafirishaji na kutoa Misaada ya Kibinadamu kwa lengo la kuboresha hali za maisha ya watu.
Bw.Laroussi amesema kwa mataifa mbalimbali ya Afrika ikiwa ni pamoja na Algeria wamekuwa wakishirikiana na jamii kubaini changamoto zinazowakumba kisha wanaziwezesha kifedha na kitaalam kukabiliana na changamoto hizo.
Social Plugin