Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NSATO MARIJANI : UMAKINI UNAHITAJIKA TUNAPOHAKIKI WAKIMBIZI DAR


Na Veronica Mwafisi, MOHA-Dar es Salaam
UHUISHAJI takwimu za wakimbizi waishio jijini Dar es Salaam na mikoa mingine nchini, unapaswa kufanywa kwa umakini mkubwa kwani unagusa usalama wa nchi. 


Mkurugenzi Msaidizi wa Uendeshaji Makambi na Makazi, kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Idara ya Huduma kwa Wakimbizi, Nsato Marijani, aliyasema hayo jana wakati akifungua mafunzo ya uhuishaji takwimu za wakimbizi. 


Mafunzo hayo yalifanyika kwenye Ukumbi wa Polisi Officer’s Mess, Oysterbay, Dar es Salaam yakihusisha watendaji wa Idara ya Huduma kwa Wakimbizi, Uhamiaji, Ofisi ya Rais, Polisi pamoja na UNHCR. 


Alisema uhuishaji takwimu utahusisha wakimbizi wote waishio jijini Dar es Salaam wenye nyaraka, walioruhusiwa kuishi nje ya kambi za wakimbizi, maeneo mengine kuanzia kesho (Novemba 4), saa 2 asubuhi hadi Novemba 7, mwaka huu. 


Alifafanua kuwa, uhuishaji huo utafanyika katika Ofisi za Shirika la Relief of Development Society (REDOSO), zilizopo eneo la Biafra, Kinondoni. 


“Matarajio ni kuhuisha takwimu za wakimbizi 243 lakini idadi hiyo inaweza kuongezeka kutokana na wakimbizi kutoka nchi mbalimbali ambao watajitokeza. 


Marijani alisema idara zote ambazo zinahusika na uhuishaji takwimu hizo, zinapaswa kufanya uhakiki huo kwa umakini mkubwa kwani zoezi hilo linagusa usalama wa nchi. 


“Jambo la msingi fanyeni kazi kwa ushirikiano na umoja kati ya watendaji wa idara za serikali na UNHCR, hakuna aliye juu ya mwingine,” alifafanua Marijani. 


Alifafanua kuwa, katika uhuishaji huo zinaweza kutokea changamoto ambapo utatuzi wake unapaswa kushirikisha viongozi na watendaji wa pande zote. 


Afisa Mkuu wa Uendeshaji, Utawala na Makambi kutoka idara hiyo, Stephen Msangi, alisema wanatarajia kuhuisha taariza za wakimbizi 231 waliojadiliwa. 


Alisema pia kua wakimbizi 12 ambao wameongezeka hivi karibuni hivyo kufikia idadi ya wakimbizi 243 walioandikishwa ambao taarifa zao zitahakikiwa na kuthibitishwa. 


Naye Monday Iddi ambaye ni Afisa Hifadhi ya Wakimbizi mkoani Kigoma, alisema lengo la uhuishaji huo ni kufahamu idadi ya wakimbizi waliopo katika mikoa mbalimbali nchini.

“Baada ya uhuishaji, taarifa zao zitakuwa katika mfumo hivyo watashindwa kujiandikisha zaidi ya mara moja, uhuishaji huu utahusisha alama za vidole na macho (mboni),” alisema. 


Mkimbizi yeyote ambaye hatajitokeza wakati wa uhuishaji takwimu taarifa zake hazitahuishwa, usajili wake utasitishwa.
Wakimbizi hao wanatakiwa kufika na nyaraka za utambulisho zikiwemo barua ya uthibitisho wa mkimbizi, usajili, kibali cha kuishi nje ya kambi, vyeti vya kuzaliwa. 


Nyaraka nyingine ni vyeti vya ndoa, hati ya kusafiria, vitambulisho vya kazi, shule, chuo na nyaraka nyingine yoyote inayomtambulisha mkimbizi ambayo inatambulika kisheria. 


Shughuli zote zinazohusiana na uhakiki wa taarifa za mkimbizi na waomba hifadhi zinatolewa bure ambapo uhuishaji huo hautahusisha wakimbizi wa mwaka 1972. 


Wakimbizi hao ni wale wanaotoka makazi ya Ulyankulu, Katumba, Mishano na waishio vijijini mkoani Kigoma.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com