Rais Magufuli ameagiza vijana wote wenye elimu ya shahada ya kwanza waliohitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) “Operesheni Magufuli” kupewa ajira katika taasisi mbalimbali za serikali.
Ujumbe huo ulitolewa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dk. Laurean Ndumbaro, katika mkutano na waandishi wa habari, jijini Dodoma jana.
“Serikali imekuwa ikiwajengea vijana uadilifu, umoja, mshikamano, moyo wa kujitolea, moyo wa uzalendo, nidhamu na ari ya kupenda kufanya kazi kwa kuwaingiza kwenye mafunzo ya Jeshi la Kujenda Taifa, hivyo kwa kutambua mchango wao, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Magufuli ameagiza wapewe ajira,” alisema.
Alitaja sifa za vijana waliohitimu JKT kuwa ni lazima wawe wametumikia kwa kipindi kisichopungua miaka miwili na kwamba wanatakiwa kuwasilisha taarifa zao binafsi, vyeti vya elimu, taaluma na vyeti vya kuhitimu mafunzo ya JKT katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kupitia barua pepe ya [email protected].
Vile vile, Dk. Ndumbaro aliwaasa waajiri wanaowarejesha kazini watumishi wa umma walioghushi vyeti vya elimu na taaluma kwa visingizio kwamba waliondolewa kimakosa au waliajiriwa kabla ya Mei 20, 2001 kwa sifa ya elimu ya darasa la saba.
“Serikali haitosita kumchukulia hatua mwajiri yeyote atakayekiuka maelekezo halali yaliyotolewa na serikali kuhusu hatua zilizochukuliwa dhidi ya watumishi walioghushi vyeti,” alionya.
Akizungumzia suala la udanganyifu na upendeleo katika upandishwaji vyeo, Dk. Ndumbaro alisema ofisi yake imebaini baadhi ya waajiri kuwasilisha taarifa za uongo Ofisi ya Rais-Utumishi ili kuwapandisha vyeo watumishi kwa lengo la kuwanufaisha baadhi yao bila kuwa na vigezo vilivyowekwa kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazosimamia utumishi wa umma.
“Ofisi yangu itaendelea kuwachukulia hatua stahiki waajiri watakaobainika kufanya udanganyifu kwa madhumuni ya kuipotosha Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili iweze kutoa vibali vya kuwapandisha vyeo watumishi isivyostahili.” Aliwataka maofisa utumishi nchini kufanya kazi kwa weledi kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma badala ya kuwa chanzo cha kero na matatizo ya kiutumishi.