Mahakama ya nchini Sudan imemkuta Rais wa zamani Omar al-Bashir na hatia ya makosa ya utakatishaji fedha na rushwa na kumhukumu kifungo cha miaka miwili gerezani.
Hiyo ni hukumu ya kwanza katika msururu wa kesi zinazomkabili al-Bashir, ambaye pia anasakwa na mahakama ya Kimataifa ya Jinai – ICC kuhusiana na mashitaka ya uhalifu wa kivita na mauaji ya halaiki yanayohusiana na mgogoro wa Darfur katika miaka ya 2000.
Hukumu ya leo inakuja ikiwa ni mwaka mmoja baada ya waaandamanaji nchini Sudan kuanzisha vuguvugu la mapinduzi dhidi ya serikali ya kimabavu ya al-Bashir.
Wakati wa miongo yake mitatu madarakani, Sudan iliwekwa kwenye orodha ya Marekani kwa kufadhili ugaidi, na uchumi wa nchi hiyo ukasambaratishwa na miaka mingi ya usimamizi mbaya na vikwazo vya Marekani.