Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Mussa Taibu, amesema hana taarifa za kukamatwa kwa ofisa wa Kitengo cha Elimu kwa Umma wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) katika himaya yake kama inavyosambazwa mitandaoni.
Kauli hiyo ilitolewa jana Jumatatu Desemba 23, 2019, na Kamanda Taibu wakati akizungumza na waandishi wa habari waliotaka kujua endapo anafahamu ofisa huyo wa LHRC amewekwa kituo gani.
“Kwa bahati mbaya sina taarifa hizi, nimeuliza wenzangu hakuna mwenye taarifa za kukamatwa kwa Tito kwenye himaya yangu.” Alisema
Alisema kuwa amewasiliana na wenzake katika himaya yake, na hakuna mwenye taarifa za kukamatwa kwa mtumishi huyo wa LHRC ambaye alikamatwa siku tatu zilizopita na bado haifahamiki anashikiliwa katika kituo kipi cha polisi.
“Inawezekana amekamatwa kwa siri na mtu mwingine asijue kwa ajili ya kufanikisha jambo fulani na siyo kila jambo linalofanyika lazima polisi ajue inategemea jambo linalozungumziwa ni la aina gani na lina usiri kiasi gani,” alisema Taibu
Magoti alichukuliwa Ijumaa iliyopita asubuhi na watu wasiojulikana wakiwa wamevalia kiraia eneo la Mwenge lakini jioni ya siku hiyo, Mambosasa alitoa taarifa akisema wanamshikilia pamoja na watu wengine watatu kwa uchunguzi wa tuhuma za jinai.
Social Plugin