Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAKOSA YA JINAI YAPUNGUA PWANI

NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
Kamanda wa polisi mkoani Pwani, (ACP) Wankyo Nyigesa amesema ,mwaka 2019 makosa ya jinai yamepungua kwa asilimia 10.5  na kuongeza kwamba hali ya usalama kwa ujumla ni shwari.

 
Aidha amesema, makosa ya kukutwa na silaha na risasi walikamata jumla ya sila 17 ikiwa ni pamoja na SMG moja na magobore 16 na risasi sita za SMG huku watuhumiwa 20  walifikishwa mahakamani kutokana na makosa hayo.

Aliweka bayana hayo wakati akielezea namna walivyojipanga kudhibiti masuala ya uhalifu wakati wa sikukuu ya krismas na mwaka mpya.

Wankyo, alieleza yaliyoripotiwa katika vituo vya polisi ni 2,074 ukilinganisha na mwaka 2018 ambapo makosa yalikuwa 2,318 hivyo yamepungua kwa makosa 244.

Alisema, kati ya makosa hayo makosa ya jinai dhidi ya binadamu ikiwemo mauaji ,kubaka ,kulawiti mwaka uliopita yalikuwa makosa 382 ,na mwaka huu yameripotiwa makosa 366 hivyo yamepungua 16 sawa na asilimia 12.

“Makosa ya kuwania mali kama vile unyang’anyi na kutumia silaha,unyang’anyi wa kutumia nguvu ,wizi wa silaha ,uvunjaji nayo yamepungua makosa 236 sawa na asilimia 19,kutoka makosa 1,240 mwaka 2018 hadi kufikia makosa 1,004 yalitokea mwaka huu”alifafanua.

Kamanda huyo alibainisha, jeshi hilo pia lilizuia magendo na uhalifu katika bandari bubu ,na kukweps ushuru zilikamatwa mafuta ya kupikia madumu 5,260 ,khanga balo 16,matairi ya pikipiki 175, mafuta ya diezel lita 320 yalikamatwa huku watuhumiwa 23 walifikishwa mahakamani.

Hata hivyo Wankyo,aliwataka wananchi washeherekee sikukuu kwa amani na utulivu na kuyataka magari yasijaze abiria kupita kiasi na madereva wafuate sheria za usalama barabarani pasipo kulewa wala kuendesha kwa mbwembwe.

Aliwaasa wamiliki wa kumbi za starehe, wasijaze watu kupita kiasi kwa matamanio ya kuongeza wateja ili kujipatia kipato.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com