Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimefungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania dhidi ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamanda Lazaro Mambosasa na Serikali kulitaka Jeshi la Polisi kumfikisha Tito Magoti na wenzake Mahakamani.
Magoti anashikiliwa na Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam tangu Ijumaa iliyopita ya Desemba 20, 2019 baada ya kumkamata akiwa Mwenge jijini Dar es Salaam.
Washtakiwa katika kesi hiyo iliyofunguliwa Jumapili na LHRC, THDRC kwa njia ya mtandao ni Kamanda wa Polisi Kanda maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa na Mwanasheria mkuu wa Serikali ya Tanzania (AG), Profesa Adelardus Kilagi.
Mkurugenzi Mtendaji LHRC, Anna Henga amesema wamechukua uamuzi huo baada ya jeshi la polisi kukaa kimya bila kuweka wazi kituo gani cha polisi alipo mfanyakazi mwenzao.
Amesema tamko la jeshi la polisi linalodai kuhusika na ukamatwaji wa Magoti linauthibitishia umma kuwa wanamshikilia ofisa huyo lakini hawaruhusu wakili wala mwajiri wake kumwona na kusimamia mahojiano yake.
Social Plugin