Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAAGIZA HOSPITALI ZOTE NCHINI KUANZISHA MFUKO WA FEDHA ZA DAWA

Na Rayson Mwaisemba, WAMJW- MWANZA
Serikali kupitia Wizara ya Afya imeagiza Waganga Wakuu wa Vituo vya Afya na Hospitali zote nchini kuanzisha mfuko wa fedha za Dawa kupitia makusanyo ya fedha za ndani, ili kuweza kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa dawa nchini.


Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu katika kikao cha uzinduzi wa Bodi mpya ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza.

“Kuanzia Vituo vya Afya, Hospitali zote za Halmashauri, za Mikoa , kuanzisha mfuko wa fedha za dawa, na vyanzo vikuu vya mifuko hii ni mapato yatokanayo na mauzo ya dawa, huduma za Maabara, huduma za mionzi” alisema Waziri @umwalimu.

Amesema, Bodi hiyo ya ushauri lengo lake kubwa ni kuhakikisha inaboresha huduma za kinga na tiba katika Hospitali, huku ikihakikisha huduma hizo zinaifikia wananchi kwa ubora na gharama nafua.

Aliendelea kusema, Sera ya Afya nchini inawataka Wananchi kuchangia huduma kwa gharama nafuu isipokuwa kwa makundi yote ya msamaha, wakiwemo Wazee, Watoto walio chini ya miaka mitano na mama wajawazito, hivyo kuwataka kuweka mifumo mizuri ili kurahisisha utoaji huduma.

Mbali na hayo, Waziri Ummy ameiagiza Bodi hiyo kuhakikisha inaboresha huduma za dharura na ajali, ili kuokoa vifo vitokanavyo weza kuepukika kupitia huduma za dharura, keisha kuwashauri kujenga jengo jipya la wagonjwa wa nje (OPD) ili kuboresha huduma kwa wananchi.

“Watu wengi wanakufa wakiwa getini Mwa Hospitali, wakati utaalamu upo, kwamba mkiboresha huduma za dharura na ajari, tunaweza kuokoa maisha ya watu wengi ” alisema Waziri @umwalimu.

Aidha, Waziri Ummy ameeleza majukumu ya Bodi hiyo ni kushauri, kutengeneza, kusimamia na kupitisha miongozo, malengo na mipango mikakati ya Hospitali kulingana na Sera na miongozo ya Serikali.

Nae Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Sekou-Toure Dkt. Dkt. Graham Mtui ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuendelea kuboresha huduma za Afya katika Hospitali hiyo kwa kuleta mashine ya uchunguzi wa figo na ini, mashine ya kusafisha figo ambazo zinatarajia kuanza kutoa huduma Januari 2020.

Kwa upande mwingine amesema, Hospitali inatarajia kupokea mashine sita ikiwemo CT Scan, X- ray yakidigitali, vifaa vya mifupa na mashine zinazosaidia kupumulia kutoka MSD.

Hata hivyo, amesema kuwa, idadi ya Wagonjwa wanaofika kupata huduma, kutoka wastani wa wagonjwa 350 kwa siku kwa mwaka 2015 hadi kufikia wagonjwa kati ya 500 mpaka 700 kwa Mwaka huu 2019, huku akiweka wazi kupunguza Rufaa za kwenda Hospitali ya Rufaa ya kanda ya Bugando kwa asilimia 50.

“Kutokana na mafanikio hayo, idadi ya wagonjwa wanaopata huduma katika Hospitali imeongezeka, kutoka wastani wa wagonjwa 350 kwa siku ambayo ilikuwa mwaka 2015, na kufikia wastani wa wagonjwa kati ya 500 hadi 700 kwa mwaka huu 2019”, alisema Dkt. Graham Mtui.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com