Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SHIRIKA LA RELI TANZANIA (TRC) KUONGEZA SAFARI ZA TRENI YA ABIRIA DAR-MOSHI

Shirika la Reli Tanzania (TRC) limesema lipo mbioni kuongeza safari za treni ya abiria kati ya Dar es Salaam na Moshi kutoka mbili kwa wiki hadi tatu.



Mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo, Masanja Kadogosa ameyasema hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari wakati akizungumzia utendaji wa shirika hilo tangu mwaka 2015.

Amesema Watanzania wamepokea kwa shauku treni hiyo, kwamba kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka wamepata maoni mengi kuhusu kuongezwa kwa safari hizo.

“Hii ni treni ya Watanzania wametoa maoni na tumeyapokea tumeyafanyia kazi, tutaona ni jinsi gani tunajipanga kuhakikisha inakwenda Moshi mara tatu kwa wiki na kurudi Dar mara tatu,”

Kadogosa pia amezungumzia ukarabati wa mabehewa ya shirika hilo na kueleza kuwa wana nia ya kuyafufua na kuyaweka katika hali nzuri ili yatumike.

Kwa sasa treni hiyo inatoka Dar es Salaam kila Ijumaa na Jumanne na Moshi kila Jumatano na Jumamosi.

Treni hiyo ambayo imeongezwa mabehewa ya abiria kutoka saba hadi nane kuanzia Jumatatu iliyopita, ina madaraja matatu.

Behewa la daraja la tatu lina uwezo wa kupakia abiria 80 waliokaa, daraja la pili kukaa abiria 60 na daraja la pili kulala abiria 36 huku nauli ikiwa Sh16,500 (daraja la tatu), Sh23,500 (daraja la pili kukaa) na Sh39,100 daraja la pili kulala.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com