Mwenyekiti wa Stand United, Dkt. Ellyson Maeja
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mwenyekiti wa Klabu ya Stand United FC' Chama la Wana' ya Shinyanga Dkt. Ellyson Maeja ametangaza kujiuzulu nafasi hiyo kwa kile alichodai kwamba amezidiwa na majukumu ya kazi zake hivyo kutokuwa na nafasi muafaka ya kupambana na kutekeleza majukumu magumu na mazito ya Klabu hiyo kwa ufanisi.
Kwa mujibu wa barua ya tarehe 12.12.2019 aliyoielekeza kwa Katibu Mkuu wa Stand United na nakala kwa wadau wa michezo mkoani Shinyanga ,Dkt. Maeja amewashukuru wanachama wa Stand United,uongozi wa serikali ya mkoa,wilaya,Mhe Salum Jambo,Mhe. Stephen Masele,CCM,TFF,Bodi ya Ligi,Baraza la wazee Shinyanga na wadau mbalimbali waliosaidia kuiunga mkono klabu kwa hali na mali.
Akizungumza na Malunde 1 blog,Dkt. Maeja amethibitisha kuandika barua hiyo na kueleza kuwa atajiuzulu rasmi Siku ya Jumapili Desemba 15,2019 kwenye mkutano mkuu wa wanachama wa Stand United utakaofanyika siku hiyo majira ya saa 10 jioni katika uwanja wa CCM Kambarage Mjini Shinyanga.
Dkt. Maeja amesema anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumwezesha kutenda majukumu ya Klabu ya Stand United kuanzia mwaka 2013 kama mwanachama wa kawaida na Juni 2015 alikuwa mjumbe wa kamati ya mkuu wa mkoa iliyoundwa na wajumbe sita kufanya maridhiano na kuhakikisha ufadhili kutoka ACACIA CO. LTD kwa klabu unapatikana na Juni 2016 akachaguliwa kwa kura nyingi kuwa mwenyekiti wa Klabu ya Stand United Fc.
"Ninawashukuru sasa hadi kufikia leo katika shida na raha,tumekuwa pamoja sina cha kuwalipa ila nawaombea kwa Mungu awape baraka tele",amesema Dkt. Maeja.
"Ninaomba kujiuzulu nafasi ya mwenyekiti Klabu ya Stand United ifikapo Desemba 15,2019. Shukrani zituendee sisi sote pale timu yetu ilipofanya vizuri na kuleta sifa kwa Wana Shinyanga kwa kushirikiana na viongozi wenzangu,wanachama,wapenzi na wadau mbalimbali.
Lakini pale yalipotokea mapungufu na pale ambapo timu haikufanya vizuri changamoto kubwa ikiwa ni ukosefu wa fedha toshelezi kwa ajili ya mishahara,ukosefu wa fedha za usajili wa wachezaji bora,ukosefu wa posho za safari na uhaba wa vifaa. Ninaomba mtuwie radhi na Mungu atusaidie kuungana kwa moyo wa upendo na kwa pamoja,kwa nguvu moja ya mkoa wetu wana Shinyanga wote kurudisha timu yetu ligi kuu",ameeleza Dkt. Maeja.
Aidha ameahidi kuwa bega kwa bega wakati wote kama mwanachama mwaminifu kusaidi klabu ya Stand United kupambana na kuleta maendeleo na furaha kwa wana Shinyanga.