Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imekabidhi eneo lenye mita mraba zaidi ya 73,000 lililopo Iyumbu jijini Dodoma kwa Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT) kwa ajili ya kuanza mradi wa ujenzi wa shule ya sekondari ya mfano.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo yaliyofanyika jijini Dodoma, Kaimu Katibu Mkuu Dkt. Ave Maria Semakafu amesema mradi huo utatekelezwa kwa kutumia Force Account ambapo Wizara ya Elimu itaunda Kamati itakayosimamia masuala yote yatakayohusu manunuzi.
"Kwa umuhimu wa mradi huu Wizara imejipanga kuhakikisha shughuli zote za manunuzi zinafanyika kwa wakati na vifaa vinavyonunuliwa vinakuwa na ubora ili kuwawezesha SUMA JKT kutekeleza mradi huu kwa ubora," amesema Kaimu Katibu Mkuu.
Dkt. Semakafu amefafanua kuwa pamoja na Wizara kusimamia manunuzi ya mradi huo, Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) wamepewa jukumu la kusimamia mradi huo ambao ujenzi wake utafanywa na Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT) na kuwataka wahusika wote hawa kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati na ubora.
Aidha, Dkt. Semakafu amewataka Chuo Kikuu cha Ardhi kuhakikisha wanatoa mahitaji halisi yanayohitajika katika utekelezaji wa mradi huo kwani kumekuwa na kawaida kwa wataalamu elekezi kutoa idadi kubwa ya mahitaji na kusababisha kubaki kwa baadhi ya vifaa ambavyo vimekuwa vikiharibika na kupoteza fedha za umma bure.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Profesa Evaristo Riwa amesema wamejipanga vyema kutekeleza mradi huo kwa kutoa mahitaji halisi na kuhakikisha unakamilika kwa wakati na ubora unaotakiwa.
Wakati huo huo Mwakishi wa SUMA JKT, Captain Deogratias Kaboya amesema wapo tayari kuanza mradi huo na kuahidi kuukamilisha kwa wakati na ubora huku akisisitiza upatikanaji wa vifaa kwa wakati.
Ujenzi wa mradi huo unahusisha ujenzi wa maabara za Fizikia, Kemia, Biolojia, Jiografia, Kompyuta na Lugha, majengo ya vyoo, majengo ya utawala, madarasa pamoja na mabweni ya wasichana na wavulana.
Majengo mengine yatakayojengwa katika mradi huo ni nyumba za walimu, maeneo ya kufulia, bwalo la chakula pamoja na kutengenezwa maeneo ya michezo na unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi sita.