Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima akizungumza kwenye mkutano wa 25 wa Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaondelea Madrid nchini Hispania.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima (mwenye tai nyekundu) akifuatilia majadiliano katika mkutano wa 25 wa Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaondelea Madrid nchini Hispania. Pembeni yake ni Afisa Misitu Mkuu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt Freddy Manyika.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima (wa pili kulia) akijadiliana jambo na ni Afisa Misitu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt Freddy Manyika. Wengine pichani kuanzia kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa na Hifadhi ya Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dkt. Agnes Kijazi.
Na Dkt. Freddy Manyika, Madrid, Hispania.
Tanzania imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka na za pamoja kushughulikia suala la mabadiliko ya tabianchi na athari zake.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mussa Sima katika mkutano wa 25 wa Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaondelea Madrid nchini Hispania.
Aliwataka wajumbe wanaoshiriki katika mkutano huo kuendelea kuchukua hatua mahsusi za kushughulikia changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
“Tunahitaji kuendeleza kasi ya kushughulikia mabadiliko ya tabianchi kwa kubainisha malengo mahususi ya kupunguza tatizo hilo kwa kuchukua hatua zote muhimu zinazohitajika” Sima alisisitiza.
Aidha ameeleza kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi tayari zimeathiri Tanzania kupitia matukio makubwa ya hali ya hewa ikiwemo mvua nyingi na kuongeza kwa joto ambavyo vinasababisha mafuriko na kusambaa kwa magonjwa ambukizi, upotevu wa mali na maisha ya wanadamu na uharibifu wa miundombinu ya barabara na madaraja katika maeneo mengi ya nchi.
Pia, Naibu Waziri alibainisha kuwa, kwa mujibu wa taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Oktaba mwaka huu imekuwa na mvua nyingi ulikinganisha na kipindi kingine kama hicho kwa karibu muongo mmoja uliopita na kuathiri sekta zote muhimu, kama vile kilimo, afya, uvuvi, mifugo, maji na afya hivyo kuongeza kwa magonjwa yakiwemo dengue na malaria.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Sima alibainisha kuwa Serikali ya Tanzania chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli, imekuwa ikichukua hatua thabiti ambazo zinachangia katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la gesijoto licha ya ukweli kuwa haikuchangia katika chanzo cha tatizo hilo.
Aliuarifu mkutano huo kuwa Tanzania imenunua rada mbili zitakazotumiwa na TMA kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utabiri hali ya hewa na majanga yatokanayo na athari za mabadiliko ya tabianchi, inaendela kupanua na kujenga mtandao wa barabara za mabasi ya mwendo wa haraka katika jiji la Dar es Salaam; inajenga reli ya viwango vya kimataifa (SGR) na kujenga bwabwa la Mwalimu Nyerere ambalo litazalisha kiasi cha 2115MW.
“Utekelezaji wa miradi hii sio tu unachochea mandeleo ya taifa na ukuaji wa uchumi, bali unachangia pia katika upunguzaji wa gesijoto ambazo zinasabaisha ongezo la joto la dunia ambalo husabaisha mabadiliko ya tabianchi” Sima aliongezea.
Pamoja na hayo, Sima aliuarifu mkutano wa Madrid kuwa, Tanzania imedhamiria kuendelea kuongeza maeneo yanayonyonya gesijoto na kutunza uoto wa asili kwa kuwa na eneo la misitu lenye ekari takiriban milioni 48, kuendelea kuongeza eneo ambalo limehifadhiwa kwa kuongeza idadi ya hifadhi za taifa na kuendelea na kampeni ya upandaji miti nchi nzima.
Alitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuunga mkono jitihada za Tanzania katika kushughulikia suala la mbadiliko ya tabainchi na kuziomba nchi zilizoendelea kuongeza juhudi zaidi katika kushughulikia suala la mabadiliko ya tabianchi kwa kutekeleza miradi na kutoa fedha na teknolojia kwa ajili ya kushughulikia tataizo hili.
Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo wa 25 wa nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaofanyika Madrid, Hispania kuanzia Tarehe 2 hadi 13, Desemba 2019 unaongozwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima na unahudhuriwa na washiriki zaidi 20,000 kutoka serikali za kitaifa, majimbo, majiji, na halmashauri, asasi za kiraia, sekta binafsi, jumuiya ya wanafanya biashara ambao wamekusanyika kujadiliana kuhusu utekelezaji wa mkataba wa Mabadiliko ya tabianchi na makubaliano ya Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi.