Mfanyakazi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) nchini Tanzania, Tito Magoti (26) na Theodory Giyani (36), wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi likiwamo la utakatishaji fedha kiasi cha Sh17milioni.
Magoti na mwenzake Theodory Giyan ambaye nii Mtaalamu wa TEHAMA wamefikishwa Kisutu na kusomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,Janeth Mtega na Wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simon akisaidiana na Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi,Faraja Nchimbi na Renatus Mkude.
Akisoma hati ya mashtaka, wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amedai Magoti na Giyani, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 137/2019.
Simon alidai katika shtaka la kwanza, Magoti na Giyani wanadaiwa kushiriki genge la uhalifu.
Amedai Tito na mwenzake katika tarehe tofauti February Mosi - Dec 17,2019 ndani ya DSM na maeneo mengine ya Tanzania, wakishirikiana na watu ambao hawapo Mahakamani kwa makusudi walishiriki makosa ya kiuhalifu ya kumiliki programu ya Kompyuta iliyotengenezwa mahususi kufanya kosa la jinai.
Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi alidai katika shtaka la pili, washtakiwa hao na wenzao ambao bado hawajafikishwa mahakamani, wanadaiwa siku na eneo hilo, wanadaiwa kumiliki programu za kompyuta kwa lengo la kutenda kosa la uhalifu.
Katika shtaka la tatu, ambalo ni kutakatisha fedha, Wakili wa Serikali Mkuu, Renatus Mkude, alidai kati ya Februari Mosi, 2019 na Desemba 17, mwaka huu, ndani ya DSM washtakiwa hao kwa pamoja walijipatia jumla ya Tsh. 17,353,535 wakati wakijua mapato hayo yametokana na nadharia ya kosa la kushiriki genge la uhalifu.
Baada ya kusomewa mashtaka yao Tito na mwenzake hawakuruhusiwa kujibu chochote kwakuwa Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi mpaka ipate kibali kutoka kwa DPP, upande wa mashtaka umedai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Hakimu Mtega ameahirisha kesi hiyo hadi January 07, 2020 itakapotajwa, Tito na mwenzake wamerudishwa rumande kutokana kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili kutokuwa na dhamana.