SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limekabidhi fedha jumla ya Shilingi Milioni 80 ili kuboresha miundombinu ya elimu na afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi na Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani.
Hii inafanyika ikiwa ni utaratibu wa TPDC wa kuwajibikaji kwa Jamii (CSR) katika maeneo yanayopitiwa na miundombinu ya bomba la gesi linaloanzia Madimba Mkoani Mtwara mpaka Kinyerezi Dar es salaam.
Kiasi cha fedha Jumla ya Shilingi Milioni 30 zimetolewa katika Shule ya Msingi Mtoni na Njianne zote zikiwa Wilaya ya kilwa kwa lengo la kuboresha Miundombinu ya elimu kwa kujenga Darasa na vyoo vya wanafunzi.
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa TPDC (Kulia) Bwn.George Seni, akikabidhi mfano wa Hundi kwa Mhe.Diwani wa Kata ya Tingi Bwn Dayani Mkenda katika Shule ya Msingi Njia nne.
Vilevile, katika kuboresha huduma za afya vijijini, TPDC imekabidhi kiasi cha Shilingi Milioni 50 kwa Halmashauri ya Kijiji cha Mwanambaya- Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani kwa ajili ya ujenzi wa Wodi ya Mama na Mtoto katika Zahanati ya Mwanambaya.
Akiongea katika hafla hiyo, Bwn Seni alisema "ili kuwa na Taifa bora lenye wananchi yenye afya na nguvu ni lazima watoto wazaliwe katika mazingira yaliyo na huduma bora za afya, ndio maana TPDC imeona vema kujenga Wodi ya mama na Mtoto ili kuwezesha huduma bora".
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa TPDC Bwn.George Seni (Mwenye Suti), akikabidhi mfano wa Hundi kwa mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Bwn.Athmani Manicho (Mhe.Diwani).
Bwn.Manicho aliahidi kutoa ushirikiano ili kuhakikisha fedha hizo zinatumika ipasavyo katika kujenga Wodi hiyo. Alieleza kuwa Wodi hiyo itahudumia jumla ya vitongoji saba (7) vilivyopo katika kijiji cha Mwanambaya vyenye wakazi zaidi ya 5,500.
Zahanati ya Mwanambaya, Mkuranga.Hapa ndipo kutajengwa Wodi ya Mama na Mtoto.
Kwa nyakati tofauti, wanufaika wa fedha hizo walitoa shukrani za dhati kwa *TPDC* kwa kuendelea kuboresha huduma za kijamii hasa katika Afya na elimu.
Akiongea katika hafla ya kukabidhi fedha za ujenzi wa darasa katika Shule ya Msingi Njia nne,Mhe.Diwani wa kata ya Tingi Bwn.Dayani Mkenda alitoa shukrani kwa TPDC kwa kuendelea kutatua kero mbalimbali za kijamii ikiwemo kuboresha miundombinu ya shule ili kuwezesha wanafunzi kusoma katika mazingira yaliyo rafiki.
"Kwa darasa hili linalojengwa kwa fedha za TPDC litawezesha wanafunzi kukaa vizuri darasani na kujisomea bila usumbufu" alionge Bwn. Dayani.
Sehemu ya wananchi waliohudhuria hafla ya kukabidhi fedha hizo .
#TPDCTUNAWEZESHA
Social Plugin