TRUMP KITANZINI LEO, AANDIKA BARUA YA HASIRA KWA SPIKA


Rais Donald Trump wa Marekani yupo katika kitisho cha kuwa rais wa 3 wa Marekani kushitakiwa pale ambapo baraza la wawakilishi la Marekani likijiandaa kupiga kura ya kihistoria ambayo itafungua milango ya mashitaka yake.



Awali, Rais Trump alisema amewekwa katika mazingira ya jaribio la mapinduzi na mashitaka ya kichawi. Katika barua yake ya kurasa sita, rais huyo alimwambia Spika wa Baraza la Wawakilishi wa chama cha Democratic, Nancy Pelosi kwamba historia itamuhukumu vikali. Barua hiyo ilitolewa ikiwa muda mfupi tu, baada ya Pelosi kutangaza kwamba baraza la wawakilishi litapiga kura leo hii.

Akiwasilisha ujumbe kwa wenzake wa chama cha Democratic, Pelosi alisema Baraza la Wawakilishi litatumia moja ya mamlaka muhimu sana ambayo limepewa kikatiba wakati wabunge watakapopiga kura kuidhinisha vifungu viwili vya mashtaka dhidi ya rais wa Marekani. 



Aidha aliongeza spika huyo kwamba katika kipindi hicho muhumi katika historia ya taifa hilo, lazima wabunge wailinde katiba ya nchi dhidi ya maadui wote wa nchi na ndani ya Marekani.

Rais Trump anakabiliwa na tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka kwa kuiagizia Ukraine kumchunguza makamo wa rais wa zamani wa Marekani Joe Biden, ambae anaongoza katika kinyang'anyiro cha kuwania urais kwa upande wa chama cha Democratic, ikitajwa kuwa kama hatua ya kumpinga katika kuwania urais katika uchaguzi wa 2020 wa Marekani.


 Trump pia anakabiliwa na shitaka la kufanya njama za kuvuruga uchunguzi wa bunge dhidi yake katika tuhuma hiyo kwa kuwazuia maafisa kutoa ushahidi wao pamoja na kuficha baadhi ya nyaraka.

 Vifungu viwili vya mashitaka vinatarajiwa kupitishwa na Baraza la Wawakilishi ambalo linadhibitiwa na chama cha Democratic. Kama mchakato utakwenda kama inavyotarajiwa kesi yake itafunguliwa Januari mwakani.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post