Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Picha : KIVULINI,POLISI & HALMASHAURI YA SHINYANGA WAADHIMISHA KAMPENI YA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA KWA KISHINDO BUTINI


Shirika la Kivulini kwa kushirikiana na halmashauri ya wilaya ya Shinyanga pamoja na jeshi la polisi wameadhimisha Kampeni ya Siku 16 za Kupinga ukatili wa kijinsia kwa kutoa elimu kwa wananchi wa kata ya Itwangi kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia katika jamii.


Kilele cha maadhimisho hayo ambayo kimkoa yamefanyika Desemba 11,2019 kwa upande wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga yamefanyika leo Jumatano Desemba 12,2019 katika kijiji cha Butini kata ya Itwangi na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi.

Kilele hicho cha maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia yameongozwa na mdahalo uliolenga kutoa elimu ya masuala ya ukatili wa kijinsia sambamba na burudani mbalimbali.

Akizungumza,Mgeni rasmi Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Mhe. Ngassa Mboje kwa niaba ya Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mhe. Jasinta Mboneko alisema suala la ukatili wa kijinsia linapaswa kukemewa na kila mtu hivyo kuwaomba wananchi wote kuwafichua watu wanaotenda uhalifu katika jamii.

Mboje alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wanaume kukaa karibu na watoto badala ya kushinda kwenye kahawa na kukosa muda wa kukaa na watoto ili kujua mienendo yao hali ambayo itachangia kukabiliana na vitendo vya ukatili.

“Unywaji wa kahawa usio na utaratibu nao sasa ni tatizo,wanaume wanatumia muda mwingi kwenye kahawa badala ya kukaa na watoto wao. Tunatengeneza kizazi cha watoto kulelewa na mama pekee wakati akina baba wapo. Wanaume hawana taarifa za watoto wao.Tubadilike tukae na watoto wetu ili tujue changamoto zao,huenda wanafanyiwa vitendo vya ukatili lakini hawajui wamweleze nani”,alisema Mboje.

Katika hatua nyingine Mboje alilipongeza na kulishukuru shirika la Kivulini kwa jitihada linazofanya kuwafikia wananchi wa pembezoni na kuwapatia elimu ya ukatili wa kijinsia ambapo kwenye maeneo ambayo shirika limefanyika jamii imebadilika na kuachana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Kwa upande,Kaimu Mkuu wa kituo cha polisi wilaya ya Shinyanga,Hussein Balige aliwataka baadhi ya viongozi wa serikali kuacha kutumia ofisi za serikali kusuluhisha kesi za jinai kama vile kesi za ubakaji na mimba za utotoni kwani kufanya vile ni kukiuka maadili ya kazi.

Naye Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto,Victoria Maro aliwakumbusha wananchi umuhimu wa kutoa taarifa za matukio ya ukatili wa kijinsia pamoja na kutoa ushahidi mahakamani kwani kesi nyingi zimekuwa zikikwama kutokana na kukosa ushahidi na wananchi kumaliza kesi kienyeji.

Nao wananchi wa kata ya Itwangi wakizungumza wakati wa mdahalo kujadili masuala ya ukatili wa kijinsia walisema kutokana na elimu waliyopata kutoka shirika la Kivulini matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto yamepungua.

“Tabia ya wanaume kuuza vyakula nyumbani na kwenda senta kuhonga wanawake wageni wanaokuja kutafuta pesa ‘Nzige’ ,kutopeleka watoto shule na wanaume kulewa pombe na kupiga wake zao imepungua sana katika eneo hili”,walisema wananchi hao. 

Hata hivyo walisema wamekuwa wakishindwa kutoa taarifa za matukio ya ukatili wa kijinsia mfano kufichua watu wanaobaka watoto na kuwapatia ujauzito kwa hofu ya kurogwa.

Afisa Tathmini na Ufuatiliaji kutoka Shirika la Kivulini,Godfrey Paschal alisema wanafanya shughuli zao katika kata tatu za halmashauri ya wilaya ya Shinyanga ambazo ni Nsalala,Nyida na Itwangi.

“Tumeamua kufanya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia katika eneo hili la Butini ikiwa ni sehemu ya vijiji ambavyo tumeunda vikundi vya wana mabadiliko ambao wamekuwa wakitoa elimu ya masuala ya ukatili wa kijinsia”,alisema Paschal.

Paschal alisema wanaendelea kushirikiana na serikali katika kupiga vita vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto huku akiwaomba wananchi kutokaa kimya pindi wanapoona dalili ama uwepo wa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Mhe. Ngassa Mboje akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya Kampeni ya Siku 16 za Kupinga ukatili wa kijinsia yaliyofanyika katika Kijiji cha Butini kata ya Itwangi halmashauri ya wilaya ya Shinyanga leo Jumatano Desemba 12,2019. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog


Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Mhe. Ngassa Mboje akilipongeza shirika la Kivulini kwa jitihada zake za kutoa elimu kwa wananchi juu ya madhara ya ukatili wa kijinsia. Kushoto ni Diwani wa kata ya Nyida Mhe. Seleman Segereti,kulia ni Kaimu Mkurugenzi halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Edward Maduhu.
Afisa Tathmini na Ufuatiliaji kutoka Shirika la Kivulini,Godfrey Paschal akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya Kampeni ya Siku 16 za Kupinga ukatili wa kijinsia yaliyofanyika katika Kijiji cha Butini kata ya Itwangi halmashauri ya wilaya ya Shinyanga leo Jumatano Desemba 12,2019.
Wakazi wa kijiji cha Butini wakimsikiliza Afisa Tathmini na Ufuatiliaji kutoka Shirika la Kivulini,Godfrey Paschal.
Meza kuu wakiwa kwenye kilele cha maadhimisho ya Kampeni ya Siku 16 za Kupinga ukatili wa kijinsia yaliyofanyika katika Kijiji cha Butini kata ya Itwangi halmashauri ya wilaya ya Shinyanga leo Jumatano Desemba 12,2019.

Wakazi wa kata ya Itwangi wakiwa kwenye kilele cha maadhimisho ya Kampeni ya Siku 16 za Kupinga ukatili wa kijinsia yaliyofanyika katika Kijiji cha Butini kata ya Itwangi.
Kaimu Mkurugenzi halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Edward Maduhu akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya Kampeni ya Siku 16 za Kupinga ukatili wa kijinsia yaliyofanyika katika Kijiji cha Butini kata ya Itwangi.
Afisa Maendeleo ya Jamii halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Deus Mhoja akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya Kampeni ya Siku 16 za Kupinga ukatili wa kijinsia yaliyofanyika katika Kijiji cha Butini kata ya Itwangi.
Kaimu Mkuu wa kituo cha polisi wilaya ya Shinyanga,Hussein Balige akitoa elimu ya ukatili wa kijinsia na kuwataka wananchi kuwa wanajitokeza kutoa ushahidi mahakamani kuhusu kesi za ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Kaimu Mkuu wa kituo cha polisi wilaya ya Shinyanga,Hussein Balige akiendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto,Victoria Maro akitoa elimu kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia. Alisema Jukumu la jeshi la polisi ni kutelekeza haki na wajibu na kuchukua taratibu za kisheria panapotokea vitendo vya ukatili wa kijinsia. 
Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto,Victoria Maro  akizungumza kwenye maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia katika kata ya Itwangi. Alisema wataendelea kuchukua hatua za kisheria kwa watuhumiwa wa vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa mimba za utotoni na watoto kuozeshwa wangali wadogo.
Wananchi wakiendelea kusikiliza nasaha mbalimbali kwenye maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia katika kata ya Itwangi.
Msanii wa nyimbo za asili Wanzigiza kutoka Isela halmashauri ya wilaya ya Shinyanga akitoa elimu ya kupinga ukatili wa Kijinsia kupitia wimbo wake wa Ukatili wa Kijinsia.
Meza kuu wakifurahia burudani iliyokuwa inaendelea.
Wanafunzi wakitoa burudani ya muziki.
Afisa Tathmini na Ufuatiliaji kutoka Shirika la Kivulini,Godfrey Paschal akiendesha mdahalo kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia kwenye kilele cha maadhimisho ya Kampeni ya Siku 16 za Kupinga ukatili wa kijinsia yaliyofanyika katika Kijiji cha Butini kata ya Itwangi halmashauri ya wilaya ya Shinyanga leo Jumatano Desemba 12,2019.
Mama Ashura mkazi wa Butini akielezea vitendo vya ukatili vinavyofanywa na wanaume katika kata ya Itwangi ikiwemo kuuza vyakula nyumbani na kwenda kutumia pesa hizo kufanya uzinzi/kuoa wanawake wengine huku familia ikiteseka.
Mzee Ikune Lya Ng'wamungu akichangia hoja wakati wa mjadala kuhusu ukatili wa kijinsia ambapo aliwakumbusha wanaume kutunza familia zao na kuepuka tabia ya kupiga wanawake huku akiwashauri wanaume wanaopigwa na wake zao watoe taarifa kwenye vyombo vinavyohusika.
Mzee Peter Shilinde maarufu ' Banana  - Ndizi' akitoa ushuhuda namna alivyokuwa anauza vyakula nyumbani na kutumia pesa kula raha na wanawake na kulewa pombe. Alisema ulevi na uzinzi vinarudisha nyuma maendeleo katika familia hivyo kuwataka wanaume kuachana na tabia hizo ili waendelee kimaisha.
Kijana Chapa Mamba akielezea hasara ya kufanya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Mkazi wa Butini akiwahamasisha wananchi kuachana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Mkazi wa Butini akichangia mada wakati wa mdahalo kujadili masuala ya ukatili wa kijinsia.
Mdahalo unaendelea.
Kundi la Ngoma la Mama Ashura likitoa burudani.
Afisa Maendeleo ya Jamii halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Aisha Omary akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya Kampeni ya Siku 16 za Kupinga ukatili wa kijinsia yaliyofanyika katika Kijiji cha Butini kata ya Itwangi.
Kundi la burudani Ngoma ya Wanunguli likitoa burudani.
Mtaalamu wa kucheza na nyoka kutoka kundi la Wanunguli akicheza na nyoka.
Wananchi wakifuatilia burudani.
Wananchi wakiwa eneo la tukio.
Maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia yakiendelea.
Maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia yakiendelea.
Msanii Eze Boy akisoma mashairi kwenye Maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
Leah akitoa burudani ya wimbo kwenye Maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
Wananchi wakiwa eneo la tukio.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Butini, Masanja Kachemba akitoa neno la shukrani kwenye maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
Wakazi wa kijiji cha Butini wakicheza na Msanii wa nyimbo za asili Wanzigiza kutoka Isela halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wakati msanii huyo akitoa elimu ya kupinga ukatili wa Kijinsia kupitia wimbo wake wa Ukatili wa Kijinsia.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com