Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, amesema leo kuwa Uturuki itawatuma wanajeshi nchini Libya, kwa kuwa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika imetoa ombi hilo.
Erdogan amesema atawasilisha mswada kuhusu ombi hilo katika bunge la Uturuki mwezi Januari.
Hapo jana, Rais Erdogan aliizuru Tunisia kujadiliana na mwenyeji wake Rais Kais Saied, kuhusu ushirikiano na uwezekano wa kusitisha machafuko nchini Libya.
Kwenye hotuba yake leo, Erdogan amesema Tunisia ilikubali kuiunga mkono serikali ya Libya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na inayoongozwa na Fayez al-Serraj.