Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HAKIMU ANASWA AKIPOKEA RUSHWA HUKU AKIJIHAMI KWA VISU SINGIDA


Na Abby Nkungu, Singida

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana  na Rushwa (Takukuru) mkoani Singida inamshikilia Hakimu mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Mtinko wilayani Singida, Bernard Kasanda (38) kwa tuhuma za kupokea rushwa ya 250,000/- taslim kutoka kwa mwananchi mmoja ili aweze kumpa upendeleo kwenye kesi iliyokuwa mbele yake.


Mkuu wa Takukuru mkoa wa Singida, Adili Elinipenda alisema mjini Singida jana kuwa licha ya kukamatwa na rushwa hiyo, mtuhumiwa pia alikutwa na visu vitano vinavyodhaniwa kutumiwa na mtuhumiwa kujihami wakati akijipatia maslahi hayo haramu.

Elinipenda alisema kuwa mtuhumiwa Kasanda alikamatwa Jumatatu Desemba 16, mwaka huu ofisini kwake baada ya kukabidhiwa maslahi hayo ya kificho ambapo mara baada ya kupokea, alizifutika kwa ustadi mkubwa ndani ya kasha la dawa ya meno la Whitedent lililoisha dawa.

"Ingawa mtuhumiwa huyu siku zote alikuwa akiwapa funguo za choo anachotumia yeye tu kwenda kuhifadhi kiasi cha fedha anachokubaliana na washitakiwa kisha kwenda kuzichukua baadae, siku hiyo alitumia mbinu nyingine tofauti ambapo alitumia kasha la dawa ya meno" alibainisha Mkuu huyo wa Takukuru.

Alieleza kuwa mtuhumiwa alipopekuliwa zaidi alikutwa na kiasi kingine cha fedha 489,100/-, visu vitano ( kimoja kikiwa kakichomeka kwenye soksi), vingine vikiwa kwenye droo ya meza yake na kwenye mkoba wake.

Mkuu huyo wa Takukuru alisema pia kuwa baada ya tukio hilo, wananchi wengine wawili waliodai wana mashauri mbele ya hakimu huyo walijitokeza na kusema nao pia walikuwa wamempatia 50,000/-na 200,000/- kama walivyo.

Alisema kuwa Taasisi hiyo inaendelea na uchunguzi wa mashauri hayo yote na kwamba umma utajulishwa baada ya kukamilika huku akisisitiza kuwa mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa kosa la kushawishi na kupokea rushwa kinyume na Kufungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya 2007. 

Wakati huo huo, Mkuu huyo wa Takukuru ametahadharisha viongozi wa Serikali na watumishi wa Umma kutojihusisha na rushwa huku akitoa angalizo kuwa Taasisi hiyo iko macho wakati wote na kwamba itaendelea kutoa elimu kwa wananchi wote katika juhudi zake za kutokomeza mchezo huo mchafu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com