Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Picha : BODI YA WAKURUGENZI AGPAHI YATUA SIMIYU...RC MTAKA AWAPONGEZA KUSAIDIA WANANCHI...'KAZI ZENU SIYO ZA KUMULIKA KWA TOCHI'


Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka ameipongeza Asasi ya kitaifa isiyo ya kiserikali ya Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) kwa kutekeleza kikamilifu miradi ya UKIMWI na kuwagusa wananchi moja kwa moja. 



Mhe. Mtaka ametoa pongezi hizo Desemba 6,2019 kwenye kikao cha Bodi ya Wakurugenzi wa AGPAHI na wadau wa UKIMWI mkoani Simiyu kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Simiyu. 


Mtaka alisema AGPAHI ni taasisi maarufu mkoani Simiyu kutokana na kwamba imekuwa ikifanya vitu vinavyoonekana katik sekta ya afya mkoani humo kwa kusaidia wananchi. 

“Nawapongeza sana AGPAHI kazi yenu inaonekana,kazi yenu haihitaji tochi ili kuona mnachofanya. Huwezi kuzungumzia mafanikio ya mkoa wa Simiyu kwenye sekta ya afya bila kuwataja AGPAHI”,alisema Mhe. Mtaka. 

“Tunazo taasisi 14 zinazojishughulisha na masuala ya afya mkoani Simiyu. Hawa wadau 13 wangefanya walau robo tu ya kilichofanywa na AGPAHI,tungekuwa na maendeleo makubwa sana katika mkoa wetu na nchi kwa ujumla”,aliongeza Mtaka. 

Mkuu huyo wa mkoa aliipongeza Bodi ya Wakurugenzi wa AGPAHI inayoongozwa na Watanzania kwa kutekeleza miradi inayogusa maisha ya wananchi huku akizitaka taasisi zingine kuiga mfano wa AGPAHI. 

“Wajumbe wa bodi ya AGPAHI mna ujasiri wa kutembelea miradi yenu kwenye mikoa kwa sababu miradi ipo.Nyinyi mna vitu,magari yenu pia yamekuwa yakitusaidia sana.Kuna baadhi ya taasisi hazina ujasiri wa kutembelea miradi kwa sababu hawana miradi,wengine kazi yao ni kugonga semina tu mwaka mzima.Hebu tufanye kazi zinazogusa wananchi tubadilishe mkoa huu”,alieleza Mtaka.

Katika hatua nyingine Mtaka alisema serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote wa maendeleo mkoani humo ili katika kuwaletea maendeleo wananchi. 

Mtaka alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wananchi kutumia kondomu ili kupunguza maambukizi ya VVU huku akibainisha kuwa kuwa upo umuhimu wa kuvunja ukimya,vijana waelezwe ukweli kuhusu UKIMWI kwamba upo na unaua hivyo wachukue tahadhari.

Kwa upande wake,Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya AGPAHI, Dkt. Edith Ngirwamungu alisema AGPAHI inatekeleza miradi yake ya UKIMWI kwa kushirikiana na serikali lengo likiwa ni kuhakikisha fedha zinazotolewa na wafadhili zinawanufaisha watanzania. 

“Tunaushukuru mkoa wa Simiyu kwa ushirikiano mnaotupatia,tunajitahidi kufanya kazi kuwafikia wananchi,AGPAHI tunataka mtoto asizaliwe na maambukizi ya VVU,hivyo tutaendelea kushirikiana na serikali katika kutoa huduma za VVU na UKIMWI kwa wananchi”,alisema Dkt. Ngirwamungu. 

Alisema AGPAHI inaendelea kuongeza ubora na upatikanaji wa huduma za matunzo na tiba za VVU kwa watoto wachanga,vijana na watu wazima katika mikoa ya Simiyu,Mwanza,Mara na Shinyanga. 

Meneja Miradi AGPAHI mkoa wa Simiyu Dkt. Julius Sipemba alisema AGPAHI inatoa huduma za VVU na UKIMWI kwa mkoa mzima wa Simiyu ambapo Mkoa wa simiyu una vituo 233 vya kutolea huduma za afya na 73 kati ya hivyo hupata usimamizi wa moja kwa moja kutoka AGPAHI.

Alisema wagonjwa wanaopata huduma kwenye vituo 73 ni sawa na 95% ya wagonjwa wote walioko kwenye vituo 233.

"AGPAHI inaboresha miundombinu kwa kujenga na kukarabati majengo, huduma za maabara kwa kununua madawa na vifaa 'iliwezesha maabara za wilaya kutoka nyota moja mpaka tatu', imetoa magari mapya kwa halmashauri 4 kati ya 6, imetoa pikipiki, msaada wa kuchunguza kifua kikuu, Saratani ya mlango wa kizazi",alieleza Dkt. Sipemba.

Aliongeza kuwa AGPAHI pia inaajiri watoa huduma wa afya kwenye maeneo yenye uhitaji na inatoa mafunzo kwa watoa huduma kulingana na miongozo ya wizara ya afya.

Wakiwa mkoani Simiyu,Wajumbe wa bodi ya  Wakurugenzi ya AGPAHI wametembelea Kituo cha Tiba na Matunzo cha Hospitali ya wilaya ya Bariadi,kukutana na Mganga Mkuu wa mkoa wa Simiyu na Mkuu wa mkoa wa Simiyu pamoja na wadau wa VVU na UKIMWI mkoani Simiyu.

 ANGALIA PICHA ZA MATUKIO HAPA CHINI
Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka akizungumza katika kikao cha Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa AGPAHI na wadau wa afya mkoani Simiyu Desemba 6,2019. Kushoto ni Mkurugenzi wa AGPAHI, Dkt. Sekela Mwakyusa,kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya AGPAHI, Dkt. Edith Ngirwamungu. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka akiipongeza AGPAHI kwa huduma za VVU na UKIMWI inazotoa mkoani Simiyu.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka akielezea namna serikali inavyoshirikiana na wadau kuwaletea maendeleo wananchi.
Katibu Tawala mkoa wa Simiyu mhe. Jumanne Sagini akiipongeza AGPAHI kwa kutekeleza miradi inayogusa wananchi mkoani Simiyu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya AGPAHI, Dkt. Edith Ngirwamungu akizungumza katika kikao cha wadau wa afya mkoa wa Simiyu. Alisema lengo la AGPAHI ni kuhakikisha hakuna mtoto anazaliwa na maambukizi ya VVU.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya AGPAHI, Dkt. Edith Ngirwamungu akizungumza katika kikao cha wadau wa afya na kueleza kuwa AGPAHI itaendelea kushirikiana na serikali katika kutoa huduma za VVU na UKIMWI.
Mkurugenzi wa AGPAHI, Dkt. Sekela Mwakyusa akielezea shughuli zinazofanywa na AGPAHI mkoani Simiyu.
Awali Mkurugenzi wa AGPAHI, Dkt. Sekela Mwakyusa akiwashukuru viongozi wa mkoa wa Simiyu kwa kuendelea kushirikiana na AGPAHI katika kutekeleza miradi ya VVU na UKIMWI. Kulia ni Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Simiyu Dkt. Gamitwe Mahazo.
Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Simiyu Dkt. Gamitwe Mahazo akizungumza katika kikao hicho.
Meneja Miradi AGPAHI mkoa wa Simiyu Dkt. Julius Sipemba  akiwasilisha mada kuhusu shughuli zinazofanywa na asasi ya AGPAHI mkoani Simiyu.
Meneja Miradi AGPAHI mkoa wa Simiyu Dkt. Julius Sipemba akielezea maeneo ambayo AGPAHI inahudumia mkoani Simiyu.
Mkuu wa wilaya ya Bariadi Mhe. Festo Kiswaga akichangia hoja wakati wa kikao cha wadau wa afya mkoani Simiyu.
Mganga Mkuu wa mkoa wa Simiyu Dkt. Festo Dugange akichangia hoja wakati wa kikao cha wadau wa afya mkoani Simiyu.
Mganga Mkuu Halmashauri ya wilaya ya Busega Dkt. Godfrey Mbagali akichangia hoja wakati wa kikao cha wadau wa afya mkoani Simiyu.
Kikao kinaendelea.
Mnufaika wa miradi inayotekelezwa na AGPAHI mkoa wa Simiyu Pendo Gidion akielezea namna huduma ya baba,mama na mtoto ilivyomsaidia ambapo aliwataka wanawake wajawazito kujitokeza kupima VVU ili kuepuka kuzaa watoto wenye maambukizi ya VVU.
Kijana James Leonard akielezea jinsi alivyonufaika na Klabu za watoto na vijana zinazohudumiwa na AGPAHI. Aliwataka vijana wajitokeze kupima afya zao na pale wanapobainika kuwa na maambukizi ya VVU basi watumie dawa za kufubaza makali ya VVU kwani kuwa na maambukizi ya VVU siyo mwisho wa maisha.
Kijana Duhye Masunga akiwashauri wazazi kuwa wawazi kwa watoto wao kama wamezaliwa na maambukizi ya VVU
Minza Manyama akiwahamasisha wazazi na walezi kuwa wawazi kwa watoto waliozaliwa na maambukizi ya VVU. Alitumia fursa hiyo kuipongeza AGPAHI kwa huduma za VVU na UKIMWI inazoendelea kutoa kwa wananchi.
Kikao cha wadau wa afya kikiendelea.
Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya AGPAHI wakiwa kwenye kikao cha wadau wa afya mkoani Simiyu.
Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya AGPAHI wakiwa kwenye kikao cha wadau wa afya mkoani Simiyu.
Kikao kinaendelea.
Awali Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya AGPAHI, Dkt. Edith Ngirwamungu (kulia) akimwelezea Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka huduma zinazotolewa na AGPAHI katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI wakati wajumbe wa bodi ya Wakurugenzi ya AGPAHI ilipotembelea ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Simiyu.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka akielezea namna mkoa wa Simiyu unavyonufaika na huduma zinazotolewa na AGPAHI mkoani Simiyu. Kushoto ni Mkurugenzi wa AGPAHI, Dkt. Sekela Mwakyusa,kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya AGPAHI, Dkt. Edith Ngirwamungu.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka akiwapongeza wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya AGPAHI kwa kusimamia vizuri asasi ya AGPAHI ambapo asasi hiyo imekuwa maarufu sana mkoani Simiyu kutokana na kugusa maisha ya wananchi.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka akiipongeza AGPAHI kwa kutekeleza miradi inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja ..alisema 'Tunahitaji local contents zaidi kutoka kwa wadau wanaotekeleza miradi katika mkoa wa Simiyu.
Mganga Mkuu wa mkoa wa Simiyu Dkt. Festo Dugange akiwashukuru AGPAHI kwa kusaidia sekta ya afya mkoani Simiyu.
Awali Mkurugenzi wa AGPAHI, Dkt. Sekela Mwakyusa akitambulisha wajumbe wa bodi ya wakurugenzi ya AGPAHI baada ya kuwasili katika ofisi ya Mganga Mkuu wa mkoa wa Simiyu Dkt. Festo Dugange (wa kwanza kulia),katikati ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya AGPAHI, Dkt. Edith Ngirwamungu.
Mganga Mkuu wa mkoa wa Simiyu Dkt. Festo Dugange akiwakaribisha wajumbe wa bodi ya wakurugenzi ya AGPAHI.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya AGPAHI, Dkt. Edith Ngirwamungu akielezea lengo ziara ya wajumbe wa bodi ya wakurugenzi ya AGPAHI mkoani Simiyu. 
Mganga Mkuu wa mkoa wa Simiyu Dkt. Festo Dugange akiwakaribisha wajumbe wa bodi ya wakurugenzi ya AGPAHI mkoani Simiyu. 
Mganga Mkuu wa mkoa wa Simiyu Dkt. Festo Dugange  akiteta jambo na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya AGPAHI, Dkt. Edith Ngirwamungu wakati wajumbe wa bodi ya wakurugenzi ya AGPAHI wakielekea katika kituo cha Tiba na Matunzo cha Hospitali ya wilaya ya Bariadi ili kuangalia namna huduma zinavyotolewa.
Kushoto ni Meneja Miradi AGPAHI mkoa wa Simiyu Dkt. Julius Sipemba  akielezea huduma zinazotolewa na AGPAHI katika Kituo cha Tiba na Matunzo cha Hospitali ya wilaya ya Bariadi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya AGPAHI, Dkt. Edith Ngirwamungu (katikati) akiuliza jambo katika Kituo cha Tiba na Matunzo cha Hospitali ya wilaya ya Bariadi.

Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya AGPAHI wakiwa katika chumba cha kutunzia mafaili ya wateja katika Kituo cha Tiba na Matunzo cha Hospitali ya wilaya ya Bariadi. Wa kwanza kulia ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya wilaya ya Bariadi,Dkt. Mwanaidi Churu akitoa maelezo kwa wajumbe wa bodi ya wakurugenzi ya AGPAHI.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya wilaya ya Bariadi,Dkt. Mwanaidi Churu akionesha kitabu cha kumbukumbu za wateja katika Kituo cha Tiba na Matunzo cha Hospitali ya wilaya ya Bariadi. 
Wajumbe wa bodi ya wakurugenzi ya AGPAHI wakiwa kwenye chumba cha dawa katika kituo cha Tiba na Matunzo cha Hospitali ya wilaya ya Bariadi. 
Wajumbe wa bodi ya wakurugenzi ya AGPAHI wakiwa nje ya kituo cha Tiba na Matunzo cha Hospitali ya wilaya ya Bariadi. 
Picha ya pamoja uongozi wa mkoa wa Simiyu,AGPAHI na wadau wa afya mkoani Simiyu.
Picha ya pamoja uongozi wa mkoa wa Simiyu,AGPAHI na  wanufaika wa miradi inayotekelezwa na AGPAHI mkoani Simiyu.
Picha ya pamoja uongozi wa mkoa wa Simiyu na AGPAHI.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com