Waasi wa kundi la ADF wameishambulia tena wilaya ya Beni Kaskazini mwashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na kuuwa watu 22 katika tarafa za Ndombi na Kamango.
Wakaazi wa wilaya ya Beni kwa mara nyingine wanahesabu maiti za wapendwa wao waliouawa kinyama na waasi wa ADF.
Mauwaji haya yanaendelea wakati jeshi la serikali linaendesha operesheni dhidi ya ADF, lakini wadadisi wa masuala ya usalama wanasema kuna uzembe katika uongozi wa jeshi hasa katika operesheni zinazotajwa na jeshi la Serikali kuwa ndio za mwisho kufanyika katika eneo hili, ili kuwatokomeza waasi wa ADF wanaowauwa watu kila uchao.
Ikumbukwe kuwa, katika ziara yake mjini Beni, na alipotangaza kwamba operesheni kabambe zitaanzishwa katika eneo hilo dhidi ya waasi wa ADF, rais Félix Tshisekedi aliwahi kuwaahidi wakaazi, kwamba waasi hao watatokomezwa kabla ya sherehe za Krismasi pamoja na mwaka mpya. Lakini ahadi hiyo inaonekana kubakia kuwa ndoto tu.
Social Plugin