Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAFUNZO YA USALAMA BARABARANI KWA WATU WENYE ULEMAVU YAFUNGWA SHINYANGA



Mkuu wa Usalama barabarani nchini, kamishina Ahmada Abdala Hamis,akiwa katika picha ya pamoja na Kamanda wa polisi mkoa wa shinyanga Sofia Jongo,mkuu wa kitengo cha usalama barabarani mkoa Athony Gwandu wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa SHIVYAWATA.
Mkuu wa Usalama barabarani nchini, Kamishina Ahmada Abdala Hamis akizungumza na walemavu mkoani Shinyanga
Baadhi ya watu wenye ulemavu mkoani Shinyanga wakimsikiliza Mkuu wa Usalama barabarani nchini, kamishina Ahmada Abdala Hamis katika hafla ya kufunga mafuzo ya siku mmoja juu ya matumizi ya sheria za usalama barabarani.

Na Salvatory Ntandu - Shinyanga
Kukosekana kwa elimu ya usalama barabarani kwa Watu wenye ulemavu mkoani Shinyanga kumetajwa kusababisha vifo kutokana na wengi wao kutokuwa na uelewa juu ya matumizi ya barabara hususani nyakati za usiku.

Hayo yamebainishwa Desemba 21,2019 na mwenyekiti wa Chama Cha Watu wenye ulemavu mkoani Shinyanga, Richard Mpongo kwenye halfa ya kufunga mafunzo ya usalama barabarani mkoani Shinyanga yaliyojumuisha watu wenye walemavu 300 kutoka halmashauri sita za mkoani humo.

“Mwaka huu wa 2019 watu wenye ulemavu watatu wamepoteza maisha kutokana na kukosa elimu ya usalama barabarani, madereva na watumiaji wengine wa barabara hawajali walemavu pindi wanapokuwa barabarani”,alisema Mpongo.

Alisema watu wasioona, viziwi ,wanaotumia baiskeli na wanaotambaa wamekuwa ndiyo wahanga wakubwa wa ajali za barabarani hususani nyakati za usiku baadhi ya madereva hawazingatii matumizi ya alama za barabarani kama vile vivuko hali ambayo imekuwa ikisababisha vifo.

Akifunga mafunzo hayo Mkuu wa Usalama barabarani nchini, kamishina Ahmada Abdala Hamis amesema Jeshi la polisi linaendelea kutoa elimu ya usalama barabarani kwa walemavu wa aina mbalimbali ili waweze kufahamu matumizi ya alama za barabarani ili kutokomeza ajali.

“Tumeamua kuwapatia elimu hii ya usalama barabarani hakikisheni mnakuwa mabalozi wema kwa wenzenu ambao bado hawajapata mafunzo haya tunaimani yatapunguza ajali zisizokuwa na lazima katika maeneo mbalimbali hapa nchini”,alisema Kamishina Hamisi.

Aliongeza kuwa ni vyema kila mtumiaji wa barabara akazingatia matumizi sahihi ya alama za barabarani hususani madereva na watembea kwa miguu ili kuhakikisha ajali zinakomeshawa hapa nchini pasipo kuwepo na shuruti.

Kwa upande wake Kaimu kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga ACP, Safia Jongo alisema watahakikisha walemavu wanalindwa ikiwa ni pamoja na kupewa haki zao zote pindi wanapotaka kutumia barabara kwa kuzingatia sheria ya usalama barabarani ya mwaka 1973.

“Tutahakikisha sheria za usalama zinafuatwa hususani katika kipindi hiki cha kuelekea katika siku kuu za krismass na mwaka mpya ambapo ajali nyingi huwa zinatokea sheria kali zitachukuliwa kwa madereva watakaobainika kuendesha vyombo vya moto bila kuchukua tahadhari kwa watu wengine”,alisema Kamanda Jongo.

Kwa upande wake Afisa ustawi wa jamii mkoa wa Shinyanga,Lydia Kwesigabo kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Shinyanga alisema serikali inatoa asilimia mbili ya mapato ya halmashauri ya ndani kama mkopo kwa watu wenye ulemavu hivyo aliziagiza halmashauri kutoa elimu ili watu wenye ulemavu wafahamu vigezo vya kuwawezesha kupata mikopo hiyo lakini pia wapewe elimu ya ujasiriamali na uundwaji wa vikundi ili wawze kujiinua kiuchumi.

Aidha aliitaka jamii kutonyanyapaa watu wenye ulemavu na halmashauri kutenga bajeti kwa ajili ya shughuli za watu wenye ulemavu na kuwapa elimu ya VVU na UKIMWI.

Mafunzo hayo ni utekelezaji wa agizo la serikali la kuwapatia elimu ya usalama barabarani kwa watu wenye walemavu wote hapa nchini ili kuzuia vifo vitokanavyo na uzembe kwa baadhi ya madereva.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com